TANZANIA-KENYA-CORONA-AFYA-USHIRIKIANO

Tanzania-Kenya: Mpaka wa Namanga wafungwa tena, kulikoni?

Madereva wa malori wanajiandaa kufanya vipimo vya Corona kwenye mpaka wa Namanga kati ya Kenya na Tanzania, huko Namanga, Kenya, Mei 12, 2020.
Madereva wa malori wanajiandaa kufanya vipimo vya Corona kwenye mpaka wa Namanga kati ya Kenya na Tanzania, huko Namanga, Kenya, Mei 12, 2020. REUTERS/Thomas Mukoya

Shughuli zimekwama kwenye mipaka miwili ya Tanzania na Kenya eneo la Namanga na Holili baada ya mipakahiyo kufungwa. Hali ambayo inaendelea kuzua sintofahamu kati ya nchi hizo mbili.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amethibitisha kufungwa kwa mpaka wa Namanga kwa upande wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya kujibu mapigo kwa kile kinachodaiwa maafisa wa Kenya kukataa kuwapokea madereva wa magari ya mizigo kutoka Tanzania ambao wamepimwa na kuonekana hawana maambukuzi ya Corona.

Madereva wa Tanzania wamelalamika kuwa vyeti vyao vimekuwa vikikataliwa wanapoingia nchini Kenya, hali ambayo imeendelea kuzua sintofahamu kati ya nchi hizo mbili jirani.

“Hakuna ushirikiano mzuri tulioupata tulipokuwa tukifuatialia kilichojiri katika mpaka wa Namanga, na sasa kuna magari zaidi ya 500 yaliyoegeshwa Arusha, Longido na mengine Namanga“ amesema mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe akihojiwa na vyomlbo vya habari.

Hivi karibuni Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe alionesha kukerwa na baadhi ya madereva wasiofuata sheria, akieleza vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na madereva wa malori waliopo safarini.

“Cheti kinachotakiwa lazima kiwe cheti chenye maana kinachotambulika na maabara inayotambulika na Shirika la Afya duniani, WHO, “ amesema waziri Kagwe.