Kiongozi mkuu wa upinzani Tanzania ashambuliwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake
Imechapishwa:
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Freeman Mbowe amevamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijini dodoma.
Msemaji wa CHADEMA Tumaini Makene, amethibitisha tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa Jumatatu.
“Ni kweli ameshambuliwa na ameumizwa,amepelekwa Hospitali kwa ajili ya matibabu. Tutatoa taarifa zaidi baaadae", amesema Makene.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Mhe.@freemanmbowetz ameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijijini Dodoma. Amekimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. Tutawapatia taarifa zaidi baadae.
CHADEMA Tanzania (@ChademaTz) June 9, 2020
Hayo yanajiri siku moja baada ya mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa utawala wa rais wa Tanzania John Magufuli kutangaza nia ya kuwania urais nchini humo wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.
Tundu Lissu kutoka chama Kikuu cha upinzani CHADEMA, kupitia mitandao ya kijamii ya chama chake amesema anaona anatosha kuleta mabadiliko nchini humo.
Lissu ambaye pia ni kiongozi wa chama chake, anasubiri uamuzi wa chama hicho ili kubaini iwapo atapambana na rais Magufuli.
Anaishi nchini Ubelgiji, alikoenda mwaka 2017 kutibiwa baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana jiji Dodoma na licha ya kusema kuwa amepona hajarudi nyumbani kwa kile anachokieleza ni kwa sababu za kiusalama.