TANZANIA-CHADEMA-SIASA-USALAMA

Shambulio dhidi ya Mbowe: Marekani yaitaka Tanzania kuwakamata wahusika

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzai nchini Tanzania, CHADEMA, Freeman Mbowe, ameshambuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzai nchini Tanzania, CHADEMA, Freeman Mbowe, ameshambuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma. Freeman Mbowe/Twitter.com

Siku moja baada ya kiongozi wa upinzani kutoka chama cha CHADEMA Freeman Mbowe kushambuliwa na watu wasiojulikana nymbani kwawke Dodoma, Marekani imetoa wito kwa serikali ya Tanzania kuanzisha uchunguzi haraka iwezekanavyo na kuwakamata wahusika.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye ukurasa wake wa Twitter Marekani kupitia ubalozi wake jijini Dar es Salaam, imelitaja shambulio la Freeman Mbowe miongoni mwa mlolongo mrefu wa matukio ya kusikitisha ya utumiaji wa nguvu na unyanyasaji yanayofanywa dhidi ya wanachama wa vyama vya upinzani.

Kiongozi mwingine wa upinzani kutoka chama hicho, Tundu Lissu alishambuliwa na kundi la watu wenye silaha alipokuwa amekaribia nyumbani kwake Dodoma tarehe 7 mwezi Septemba 2017. Lakini mpaka sasa uchunguzi kuhusu shambulio la mwanasiasa huyo haujazaa matunda yoyote.

Mapema wiki hii Tundu Lissu ambaye ni mkosoaji mkubwa wa utawala wa rais wa Tanzania John Magufuli alitangaza nia ya kuwania urais nchini humo wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.

Tundu Lissu kutoka chama Kikuu cha upinzani CHADEMA, kupitia mitandao ya kijamii ya chama chake alisema anaona anatosha kuleta mabadiliko nchini humo.

Lissu alisema anasubiri uamuzi wa chama chake ili kubaini iwapo atapambana na rais Magufuli.

Anaishi nchini Ubelgiji, alikoenda mwaka 2017 kutibiwa baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana jiji Dodoma, na licha ya kusema kuwa amepona hajarudi nyumbani kwa kile anachokieleza ni kwa sababu za kiusalama.

Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, wakiwa kwenye moja ya mikutano ya chama hicho wakati wa kampeni za urais.
Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, wakiwa kwenye moja ya mikutano ya chama hicho wakati wa kampeni za urais. RFI