TANZANIA-SIASA-USALAMA

Upinzani Tanzania: Tuko tayari kushiriki uchaguzi licha ya vitimbi tunavyofanyiwa

Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, wakiwa kwenye moja ya mikutano ya chama hicho wakati wa kampeni za urais.
Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, wakiwa kwenye moja ya mikutano ya chama hicho wakati wa kampeni za urais. RFI

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vinasema vitashiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba licha ya madai ya kunyanyaswa na vyombo vya Dola na kutokuwa na imani na Tume ya Uchaguzi.

Matangazo ya kibiashara

Wiki hii, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe alikamatwa na baadaye kuachiliwa huru.

Vyama vya upinzani nchini Tanzania kwa muda mrefu vimekuwa vikililia kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Chama kikuu cha Upinzani nchini humo cha CHADEMA kimesema kitang'ang'ana kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, huku Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia akionyesha wasi wasi wake kuhusu uchaguzi huo.

Chama cha ACT Wazalendo kinasema wapo tayari kwa Uchaguzi licha ya tume iliyopo.

“Sie uchaguzi tutashiriki kwa hali yoyote ile hata kama watakwenda hivyo na tume yao hiyo na sheria zao hizo tutapambana tu katika uchaguzi, “ amesema Haji Duni, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT visiwani Zanzibar.

Kwa upande wake Chama kilichopo Madarakani CCM kinasema “kila kitu kipo sawa, zingine ni porojo”.

Kwa Mujibu wa Katiba ya Tanzania, Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi huteuliwa na Rais.

Vyama mbalimbali nchini Tanzania vinaendelea na michakato ya ndani ya kutafuta wagombea kuelekea uchaguzi huu, huku kiongozi mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe pamoja na viongozi wengine wa chama hicho wakiwa Kilwa Kusini,  mkoani Lindi walikamatwa na polisi wakiwa katika mkutano wa ndani wakidaiwa kufanya maandamano yasiyo na Kibali.