BURUNDI-NKURUNZIZA-SIASA-USALAMA

Pierre Nkurunziza azikwa katikati mwa Burundi

Le cercueil de Pierre Nkurunziza lors de ses funérailles au stade de Gitega, Burundi, le 26 juin 2020.
Le cercueil de Pierre Nkurunziza lors de ses funérailles au stade de Gitega, Burundi, le 26 juin 2020. TCHANDROU NITANGA / AFP

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza aliyefariki ghafla tarehe 8 mwezi huu katika hospitali ya mkoa wa Karusi, amezikwa leo kwenye makaburi ya mashujaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Gitega.

Matangazo ya kibiashara

Wananchi wa Burundi pamoja na wageni waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi hiyo wamehudhuria mazishi hayo.

Hafla ya kumuaga Nkurunziza ilifanyika katika uwanja wa soka wa Ingoma, katika mji mkuu wa nchi hiyo Gitega, kabla ya mazishi kufanyika mita kadhaa na uwanja huo.

Kiongozi huyo wa zamani wa Burundi, aliyeongoza taifa hilo kwa miaka 15, alifariki dunia Juni 8 akiwa na umri wa miaka 55.

Kifo chake kilikuja muda mfupi baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu na alikuwa akabidhi madaraka mwezi Agosti, lakini ripoti nchini humo zinasema alipata mshtuko wa moyo na kupoteza maisha.

Raia waliotakiwa kuhudhuria hafla ya mazishi ya hayati Nkurunziza walikuwa wamevaa nguo za rangi nyeupe kulingana na ombi la serikali.

Pierre Nkurunziza amewaacha watoto watano, na mkewe Denise Bucumi alimsifu mume wake kwa mema aliyotendea nchi ya Burundi na kwamba 'mwisho wake umekuwa mwema na kufa kifo cha amani'.

Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, yamekuwa yakiomboleza na wananchi wa Burundi kwa kupeperusha nusu mlingoti bendera za nchi zao na ile ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waliompenda Nkurunziza wanamkumbuka kama kiongozi aliyeongoza umoja wa wananchi wa taifa hilo la Afrika ya Kati baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini wakosoaji wake wanasema alikiuka haki za binadamu na kuwazima wapinzani wake.