BURUNDI-CORONA-AFYA

Évariste Ndayishimiye: Corona ni adui wa umma namba moja

Évariste Ndayishimiye akila kiapo na kuwa Rais mpya wa Burundi, katika uwanja wa soka wa Ingoma, Gitega, Juni 18, 2020.
Évariste Ndayishimiye akila kiapo na kuwa Rais mpya wa Burundi, katika uwanja wa soka wa Ingoma, Gitega, Juni 18, 2020. Tchandrou NITANGA / AFP

Msimamo wa Burundi umeanza kubadilika katika mapambano dhidi ya janga hatari la Corona, ambapo rais mpya wa nchi hiyo Évariste Ndayishimiye amewataka raia kuhakikisha ugonjwa huo umetokomezwa nchini Burundi.

Matangazo ya kibiashara

Mamlaka nchni Burundi ilikuwa imepuuzia ugonjwa huo tangu ulipozuka nchini humo, viongozi wakibaini kwamba taifa la Burundi na raia wake wanalindwa na Mwenyenzi Mungu.

Hali hiyo ilionekana wakati wa mechi za soka ambapo mashabiki na watazamaji walikuwa wakitazama mechi hizo bila kuwepo na hatua za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo, hususan uvaaji barakoa na mtu kuwa kwenye umbali wa mita moja na mwengine, wakati nchi zingine duniani zilikuwa zimesitisha michuano ya aina mbalimbali kutokana na janga hilo la Covid-19.

Hata hivyo wakati wa kampeni za uchaguzi maelfu ya watu walionekana wakifuatilia kampeni hizo bila sawi wasi wowote, huku viongozi wakiunga mkono.

Jumanne wakati mawaziri wapya 15 walikuwa wakila kiapo, rais Évariste Ndayishimiye aliwatolea wito raia wake kuhakikisha ugonjwa wa Corona umetokomezwa nchini Burundi, huku akitangaza kuwa bei ya sabuni imepunguzwa kwa asilimia 50 na bei ya maji katika mikoa yote ya Burundi imepunguzwa.

Amewataka wafanyabiashara na viwanda vya sabuni kutekeleza hatua hiyo na kwamba sehemu iliyopunguzwa italipwa na serikali.

Rais Ndayishimiye amesema sasa vipimo vya Corona ni bure, na madaktari wanatoa huduma ya matibabu bure.

"Sielewi kwa nini watu wenye dalili za ugonjwa wa Corona wanakataa kwenda kufanya vipimo vya ugonjwa huo au kutibiwa, ili wasiambukizi wengine, " amesema rais Évariste Ndayishimiye.

Kuanzia hivi sasa ikiwa mtu atakataa kwenda kufanya vipimo na ana dalili za ugonjwa huo, hii itamaanisha kuwa anataka kuambukizwa wengine kwa makusudi. Kwa hiyo atachukuliwa kama adui na ataadhibiwa kulingana na ukubwa wa kosa hilo, " ameongeza rais wa Burundi.

"Tutaweka timu za maafisa wa afya ambao wataendesha zoezi la vipimo vya Covid-19 katika mikoa yote ya nchi, kabla ya kuzindua kampeni za vipimo kwa raia popote pale ambapo kutapatikana visa vya maambukizi, " amebaini rais Évariste Ndayishimiye.