BURUNDI-UHURU-USALAMA-SIASA

Burundi yaadhimisha miaka 58 ya Uhuru

Kiongozi wa wanaharakati waliotetea uhuru wa Burundi, Mwanamfalme Louis Rwagasore.
Kiongozi wa wanaharakati waliotetea uhuru wa Burundi, Mwanamfalme Louis Rwagasore. Youtube.com

Wananchi wa Burundi hii leo wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 58 toka taifa hilo lilipojipatia uhuru wake toka kwa wakoloni wa Ubelgiji Julai 1, 1962, wakati huu taifa hilo lina rais mpya Evariste Ndayishimiye aliyechukua mikoba ya mtangulizi wake Pierre Nkurunziza, aliyefariki dunia Juni 8, 2020 kwa maradhi ya moyo.

Matangazo ya kibiashara

Mwaka moja kabla ya uhuru kulikuwa na uchaguzi wa kwanza chini ya usimamizi wa Umoja Mataifa, na chama mshindi kilikuwa UPRONA kilichoongozwa na mwanamfalme Mtutsi Louis Rwagasore aliyemwoa mwanamke wa Kihutu na chama kiliunganisha pande zote mbili.

Lakini miezi michache baadaye Rwagasore aliuawa na chama chake kilitengana kufuatana na ukabila.

Mwaka 1962 Umoja wa Mataifa uliamua kuipa Ruanda-Urundi uhuru kamili, lakini kila nchi pekee.

Sherehe rasmi zimefanyika kwenye uwanja wa soka wa mashujaa mjini Bujumbura.

Siku hii ya leo inafika wakati wanasiasa wengi wa upinzani wakiwa ukimbizini, nje ya nchi, bila kusahau watu zaidi ya 300,000 ambao walitoroka makaazi yao na kukumbilia, wengi wao katika nchi jirani za DRC, Rwanda, Uganda, Kenya, Zambia na Tanzania.

Hata hivyo katika hotuba yake baada ya kula kiapo rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye alitolea wito raia wa Burundi waliotoroka makazi yao kufuatia machafuko ya mwaka 2015, kurejea nchini na wahisi kwamba wanarudi nyumbani kushirikiana na wenzao Warundi waliobaki nchini kwa kulijenga taifa.

Alionya mtu yeyote kumnyanyasa mwenziye kwa sababu za kisiasa, kidini na kusema kuwa atachuliwa hatua, huku akibaini kwamba Burundi inawahitaji raia wake kwa kuleta maendeleo nchini katika nyanja mbalimbali.

Hayo yanajiri wakati Jumanne wiki hii rais Ndayishimiye aliwataka mawaziri wapya kutekeleza majukumu yao vilivyo bila ubaguzi wowote kwa sababu mbalimbali na kufikiria kuwa iwapo watashindwa kuna watu wengine ambao wako tayari kuchukuwa nafasi zao.

Rais Ndayishimiye alisema atahakikisha katika utawala wake visa vya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi vinakomeshwa nchini Burundi.