KENYA-CORONA-AFYA

Rais Uhuru kulihutubia taifa wakati maambukizi yapindukia zaidi ya 7,800

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Kenyagvt

Wakenya wanasubiri hotuba ya rais Uhuru Kenyatta baada ya kumalizika kwa makataa ya watu kutotembea na kufungwa kwa miji ya Nairobi na Mombasa kutokana na janga la virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Raia wengi nchini humo wanaonekana wanataka marufuku hayo kuondolewa, licha ya kuendelea kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Wizara ya afya inasema watu zaidi ya Elfu Saba na Mia nane wameambukizwa virusi hivyo tangu mwezi Machi.

Rashid Aman, Katibu katika wizara hiyo ya afya anasema ongezeko la maambukizi ni kwa sababu watu hawazingatii masharti ya watalaam wa afya.

Idadi ya wagonjwa wa Covid-19 imeongezeka kwa kasi tangu mgonjwa wa kwanza aripotiwe mwezi Machi mwaka huu na idadi ya wagonjwa inatarajiwa kuongezeka kutokana na kuendelea kwa upimaji wa virusi hivyo.

Wakati serikali nchini humo inapoendelea kutafakari kufungua uchumi wa nchi hiyo na kuwaruhusu watu kuanza kutembea kutoka kaunti moja kwenda nyingine, wadau wa utalii sasa wanasema wanategemea watalii wa ndani na wale kutoka nchi jirani kusaidia kuinua sekta hiyo ambayo imepata hasara kubwa.

Nchini Kenya, hoteli na migahawa imeruhusiwa kufunguliwa lakini hoteli za kitalii zimebaki tupu kwa kukosa wageni, huku wafanyikazi wakipoteza kazi zao.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ya bara Afrika yenye vivutio vingi vya utalii, lakini kutokana na janga la Corona, imefunga anga lake, huku matumaini sasa yakiwa ni kwa watalii wa ndani na wale kutoka nchi jirani.