UGANDA-RWANDA-USHIRIKIANO

Uganda yafutilia mbali madai ya kuwanyanyasa raia wa Rwanda

Marais wa Rwanda na Uganda, Paul Kagame na Yoweri Museveni, mwaka 2018 huko Entebbbe.
Marais wa Rwanda na Uganda, Paul Kagame na Yoweri Museveni, mwaka 2018 huko Entebbbe. Michele Sibiloni / AFP

Serikali ya Uganda imekanusha madai ya serikali ya Rwanda kuwa, Kampala imeendelea kuwakamata raia wake na kuwanyima haki ya kupata mawakili.

Matangazo ya kibiashara

Katibu katika wizara ya mambo ya nje, Balozi Patrick Mugoya amesema hamna raia yeyote wa Rwanda aliyeko kizuizini.

Kwa muda nchi hizo jirani zimekuwa zikizozania mpaka wa Gatuna  na mkutano wa mwisho wa marais wa nchi hizo mbili na mataifa mengine jirani ,ulionekana kutuliza mzozo huo.

Serikali ya Rwanda inaishutumu Uganda kuwanyanyasa raia wake wanaoishi ama kutembelea nchini Uganda na pia nchi hiyo kusaidia makundi ya waasi wanaotaka kuangusha utawala wa Rwanda.

Uganda immendelea kanusha hayo na kwa upande wake kuishutumu Rwanda kutumia ardhi yake kwa ujasusi.

Kuvunjika kwa uhusiano kati ya Rwanda na Uganda kulianza mwishoni mwa mwezi wa pili mwaka huu ambapo mamlaka ya mapato ya Rwanda ilifunga kituo cha mpaka wa Gatuna na kusimamisha maroli ya mizigo kutotumia tena mpaka huo kutokana na shughuli za ujenzi wa kituo hicho.

Hali hii ilisababisha biashara iliyokuwepo baina ya Rwanda na Uganda kukwama huku bei za bidhaa kutoka Uganda kupanda mara dufu katika masoko ya Rwanda.