UGANDA-RWANDA-USHIRIKIANO

Uganda yawaachilia huru Wanyarwanda 12

Rais wa Angola Joao Lourenço amezungukwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni (kushoto) na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame (kulia) baada ya kusaini makubaliano ya kutuliza uhasama Agosti 21, 2019.
Rais wa Angola Joao Lourenço amezungukwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni (kushoto) na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame (kulia) baada ya kusaini makubaliano ya kutuliza uhasama Agosti 21, 2019. JOAO DE FATIMA / AFP

Serikali ya Uganda imewaachia huru raia 12 wa Rwanda katika juhudi za kuboresha uhusiano kati ya mataifa hayo jirani, ambayo yalikuwa na mvutano kwa miezi kadhaa.

Matangazo ya kibiashara

Mwezi uliopita pia, Uganda iliwaachia raia wengine 130 wa Rwanda waliokuwa wanazuiliwa kwa muda nchini humo, hii ikiwa mojawapo ya makubaliono ya mkutano wa mwisho wa marais wa nchi hizo na mataifa mengine jirani ya kusuluhisha mzozo kati ya Rwanda na Uganda.

Mapema wiki hii Serikali ya Uganda ilikanusha madai ya serikali ya Rwanda kuwa, Kampala imeendelea kuwakamata raia wake na kuwanyima haki ya kupata mawakili.

Awali Katibu katika wizara ya mambo ya nje, Balozi Patrick Mugoya alisema hamna raia yeyote wa Rwanda aliyeko kizuizini.

Kwa muda nchi hizo jirani zimekuwa zikizozania mpaka wa Gatuna  na mkutano wa mwisho wa marais wa nchi hizo mbili na mataifa mengine jirani, ulionekana kutuliza mzozo huo.

Kuvunjika kwa uhusiano kati ya Rwanda na Uganda kulianza mwishoni mwa mwezi wa pili mwaka huu ambapo mamlaka ya mapato ya Rwanda ilifunga kituo cha mpaka wa Gatuna na kusimamisha maroli ya mizigo kutotumia tena mpaka huo kutokana na shughuli za ujenzi wa kituo hicho.

Hali hii ilisababisha biashara iliyokuwepo baina ya Rwanda na Uganda kukwama huku bei za bidhaa kutoka Uganda kupanda mara dufu katika masoko ya Rwanda.