BURNDI-USALAMA-SIASA

Magavana wapya wateuliwa Burundi, mashirika ya kiraia yakosoa

Evariste Ndayishimiye, rais mteule wa Burundi, hapa alikuwa mjini Gitega, wakati wa zoezi la upigaji kura Mei 20, 2020.
Evariste Ndayishimiye, rais mteule wa Burundi, hapa alikuwa mjini Gitega, wakati wa zoezi la upigaji kura Mei 20, 2020. AFP

Serikali mpya ya Burundi imewateua magavana wapya, ambao wameidhinishwa na bunge la Senate, lakini uteuzi huo unaleta hofu miongoni mwa mashirika ya kiraia.

Matangazo ya kibiashara

Uteuzi huo wa Magavana 18 pamoja na Meya wa jiji la Bujumbura, ulifanywa na rais Evariste Ndayishimiye na miongoni mwa Magavana hao ambao kazi yao ni kuongoza mikoa ya nchi hiyo na wanaripoti moja kwa moja kwa rais wa nchi hiyo.

Nafasi hizo zilikuwa zimetengewa raia wa kawaida lakini sasa baadhi ya Magavana ni ni maafisa wa juu wa polisi na jeshi.Mikoa ambayo imewapata magavana kutoka jeshi na Polisi ni Cibitoke, Kayanza, Bururi, Mwaro na Manispaa ya jiji la Bujumbura.

Mara ya mwisho kufanyika kwa uteuzi wa Wanajeshi kuwa Magavana ilikuwa ni miaka 20 iliyopita katika taifa hilo la Afrika ya Kati lililokuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1993-2006.

Pacifique Nininahazwe, mmoja wa viongozi wa Mashirika ya kiraia anayeishi nje ya nchi, anasema uteuzi wa askari na maafisa wa polisi kwenye nafasi za uongozi wa mikoa ni kuwanyima haki kamili raia ambao wameendelea kuishi katika hali hofu kutokana na visa vya mauaji na vimekuwa vikiendelea kuripotia katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Hata hivyo, kinyume na Katiba ya mwaka 2005, katiba mpya nchini humo haikatazi, maafisa wa usalama kuteuliwa katika nyadhifa hizo, huku afisa wa serikali akisema hii inatoa nafasi kwa viongozi wenye vipaji waliohudumu katika jeshi kuonesha uwezo wao kama alivyo Meya mpya wa jiji la Bujumbura Jenerali Jimmy Hatungimana, aliye kuwa mkuu wa idara ya uhamiaji.

Ukosoaji mwingine kwenye uteuzi huu ni kuwepo kwa idadi ndogo ya Watutsi, katika uteuzi huu ambao kuna Magavana watatu Watutsi na 15 Wahutu kinyume na katiba inayohimiza usawa katika nyadhifa za uteuezi.