KENYA-CORONA-AFYA

Idadi ya maambukizi yapindukia zaidi ya 13,000 nchini Kenya

Maambukizi ya virusi vya Corona nchini Kenya yanaendelea kuongezeka na sasa yamefikia zaidi ya Elfu 13, huku mamia ya watu wakitangazwa kuambukizwa kila siku, hali inayoshuhudiwa baada ya kulegezwa kwa masharti na kufungua uchumi wa taifa hilo.

Moja ya mita ya maeneo ya Kibera jijini Nairobi, Kenya, Mei 22, 2020, ambapo watu wametakiwa kuvaa Barakoa katika kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona.
Moja ya mita ya maeneo ya Kibera jijini Nairobi, Kenya, Mei 22, 2020, ambapo watu wametakiwa kuvaa Barakoa katika kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona. REUTERS/Baz Ratner
Matangazo ya kibiashara

Upimaji wa maambukizi hayo umelenga pia taasisi za umma kama, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia Mamlaka ya utozaji ushuru KRA, ambapo wafanyakazi wamekuwa wakipimwa baada ya kuripotiwa kwa visa vya maambukizi.

Wafanyakazi katika Ofisi hizo za serikali walipunguzwa, wengi wakihimizwa kufanya kazi wakiwa nyumbani, huku idadi ya wageni wanaotembelea Ofisi hizo ikipunguzwa.

Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, baada ya kuripotiwa kwa kisa cha maambukizi katika Ikulu ya Nairobi tarehe 15 mwezi Juni, amehamishia kazi zake katika Jumba la Harambee liliko na Ofisi yake, katikati ya jiji la Nairobi.

Wasaidizi wa rais Kenyatta ambaye kwa sasa anaishi katika makaazi yake ya kibinafasi wamepunguzwa hasa wazee, lakini wafanyakazi wa Ikulu hawaruhusiwi kuondoka katika eneo hilo na yeyote anayekutana na rais, lazima apimwe.

Mikutano yote mikubwa kwa sasa inafanyika katika jumba la KICC jijini Nairobi.