TANZANIA-SIASA-USALAMA

Mashirika yaliyofutwa kwenye orodha ya waangalizi wa uchaguzi Tanzania yatoa malalamiko yao

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali nchini Tanzania yameandikia barua Tume ya Uchaguzi nchini humo kutaka maelezo ya kwanini, yameondolewa katika orodha ya waangalizi wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba.

Pilika pilika za uchaguzi nchini Tanzania zinaendelea.
Pilika pilika za uchaguzi nchini Tanzania zinaendelea. REUTERS/Emmanuel Herman
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya mashirika hayo pia kuondolewa katika mashirika zaidi ya 200 yanayotarajiwa kutoa elimu ya upigaji kura kwa wananchi.

Miongoni mwa mashirika hayo yaliondolewa katika orodha hiyo ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pamoja na muungano wa mashirika ya kiraia nchini humo.

Hata hivyo vyama vya upinzani nchini Tanzania vinasema vitashiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba licha ya madai ya kunyanyaswa na vyombo vya Dola na kutokuwa na imani na Tume ya Uchaguzi.

Chama kikuu cha Upinzani nchini humo cha CHADEMA kimesema kitang'ang'ana kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, huku Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia akionyesha wasi wasi wake kuhusu uchaguzi huo.

Chama cha ACT Wazalendo kinasema wapo tayari kwa Uchaguzi licha ya tume iliyopo.

Kwa upande wake Chama kilichopo Madarakani CCM kinasema “kila kitu kipo sawa, zingine ni porojo”.

Imesalia miezi mitatu kufanyika uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na madiwani nchini Tanzania ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.