Waumini wa dini mbalimbali wakaribisha hatua ya serikali ya kufungua maeneo ya kuabudu Kenya
Makanisa kwa mara ya kwanza yamefunguliwa tangu jana Jumapili nchini Kenya, baada ya kufungwa mwezi Machi kutokana na janga la virusi vya Corona.
Imechapishwa:
Waumini walirejea katika maeneo yao ya kuabudu chini ya masharti ya Wizara ya afya, katika taifa hilo ambalo linaendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo ambapo watu zaidi ya Elfu 13 sasa wameambukizwa.
Waumini wa makanisa mbalimbali waliojitokeza wakivalia barakoa, wakikaa umbali wa mita moja, ukiwa ni utaratibu mpya, katika mapambano dhidi ya Corona.
"Mtu anapokuja kwenye ibada lazima avae barakoa alafu akiingia kanisani lazima aoshe mikono na kukiwataka waumini kukaa umbali wa mita moja na mwengine na kwenye ibada zetu hakuna kusalimiana walwa kusogeleana kulingana na sheria ambazo zimeekwa, “ amesema Titus Buyengo, mchungaji wa Kanisa la Word of Life, mtaani Kayole jijini Nairobi.
Baada ya miezi mitatu ya kutoingia Kanisani, waumini wameelezea furaha yao kurejea tena katika eneo maeneo ya kuabudu.
Siku ya leo ninafuraha na kushukuru serikali kuweza kuturuhusu kukutana tena kama kanisa, hakika nilipokuwa kule nyumbani nilikuwa nakosa ule ushirika wa kuweza kuwa pamoja kama jamii ya kristo, ” amesema Night Msukh, mmoja wa waumini.
Serikali ya Kenya imeagiza kuwa maeneo ya kuabudu yanayofunguliwa, yasiwe na watu 100, ibada zisidizi saa moja na watu wenye umri wa miaka zaidi ya 58, hawaruhusiwi kwenda katika maeneo ya ibada.
Ijumaa iliyopita, baadhi ya misikiti ilifunguliwa lakini mingine imesalia kufungwa.
Maeneo ya ibada yanapofunguliwa, viongozi wa dini mbalimbali na wauamini wao, wana matarajio kuwa hivi karibuni serikali italegeza zaidi masharti ya watu kwenda katika maeneo ya kuabudu.