UGANDA-USALAMA-SIASA

Museveni apewa ridhaa na chama chake kuwania urais kwa muhula wa sita

Rais Yoweri Museveni anakubali ombi kutoka kwa Wabunge wa mkoa wa Buganda kupeperusha bendera ya chama tawala cha NRM katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021.
Rais Yoweri Museveni anakubali ombi kutoka kwa Wabunge wa mkoa wa Buganda kupeperusha bendera ya chama tawala cha NRM katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021. .gov.ug jpg

Chama tawala nchini Uganda cha NRM kimemuidhinisha Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni kuongoza taifa hilo kwa muhula wa sita mfululizo.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake, chama cha NRM kimesema kuwa Rais Museveni amepata saini za kutosha kumuwezesha kugombe kiti cha urais.

Msemaji wa chama cha NRM Rogers Mulindwa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Rais Museveni "ameidhinishwa na chama kama mgombea wake " katika uchaguzi ujao.

Museveni anatarajiwa kukabiliana na mbunge wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayefahamika kwa jina la Bobi Wine, ambaye anatarajiwa kuwania kiti cha urais.

Mwaka 2017 bunge la Uganda lenye wabunge wengi wa chama cha NRM- liliondoa ukomo wa umri wa rais, jambo lililokuwa kikwazo kwa rais Museveni kuwania tena kiti cha urais, na hivyo kumuwezesha kuwania urais.

Iwapo Rais Museveni atachaguliwa kuiongoza Uganda kwa muhula mwingine wa sita wa miaka mitano, atakuwa ameliongoza taifa la Afrika Mashariki kwa miaka arobaini, na anaweza kuongoza miaka zaidi iwapo atataka kufanya hivyo.

Rais Museveni ameliongoza taifa la Uganda kwa miaka 34, akiwa ni rais wa tatu barani afrika kuwa madarakani kwa miaka mingi zaidi, baada ya Rais wa Guinea Equatorial Teodoro Obiang ambaye amehudumu kwa miaka 41 akifuatiwa na rais wa Cameroun Paul Biya, ambaye amehudumu kwa miaka 38.

Ingawa tarehe rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda haijatangazwa, inatarajiwa kuwa uchaguzi huo utafanyika Februari 2021, kulingana na vyanzo vilivyo karibu na utawala.