UGANDA-WINE-SIASA-USALAMA

Mwanasiasa pia mwanamuziki Bobi Wine aunda chama kipya kuelekea Uchaguzi Mkuu Uganda

Mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayejulikana kwa jina la Bobi Wine kupitia muziki wa Pop baada ya kukamatwa na polisi nchini Uganda.
Mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayejulikana kwa jina la Bobi Wine kupitia muziki wa Pop baada ya kukamatwa na polisi nchini Uganda. AFP PHOTO/Michele SIBILONI

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi ,maarufu kama Bobi Wine, amezindua chama kipya kinachojulikana kama National Unity Platform kuelekea Uchaguzi Mkuu mapema mwaka 2021. Chama amabacho anasema kitakuwa chini ya vuguvugu aliloanzisha la People Power.

Matangazo ya kibiashara

Hayo yanajiri siku chache baada ya Chama tawala nchini Uganda cha NRM kumuidhinisha Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni kuongoza taifa hilo kwa muhula wa sita mfululizo.

Museveni anatarajiwa kukabiliana na mbunge wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayefahamika kwa jina la Bobi Wine, ambaye anatarajiwa kuwania kiti cha urais.

Mwaka 2017 bunge la Uganda lenye wabunge wengi wa chama cha NRM, liliondoa ukomo wa umri wa rais, jambo lililokuwa kikwazo kwa rais Museveni kuwania tena kiti cha urais, na hivyo kumuwezesha kuwania urais.

Iwapo Rais Museveni atachaguliwa kuiongoza Uganda kwa muhula mwingine wa sita wa miaka mitano, atakuwa ameliongoza taifa la Afrika Mashariki kwa miaka arobaini, na anaweza kuongoza miaka zaidi iwapo atataka kufanya hivyo.

Rais Museveni ameliongoza taifa la Uganda kwa miaka 34, akiwa ni rais wa tatu barani afrika kuwa madarakani kwa miaka mingi zaidi, baada ya Rais wa Guinea Equatorial Teodoro Obiang ambaye amehudumu kwa miaka 41 akifuatiwa na rais wa Cameroun Paul Biya, ambaye amehudumu kwa miaka 38.

Ingawa tarehe rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda haijatangazwa, inatarajiwa kuwa uchaguzi huo utafanyika Februari 2021, kulingana na vyanzo vilivyo karibu na utawala.