Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa aaga dunia
Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo wakati alipokuwa anapata matibabu Hospitalini jijini Dar es salaam baada ya kulazwa.
Imechapishwa:
Kifo cha rais huyo za wa zamani aliyekuwa na umri wa miaka 81 na aliyeongoza nchi hiyo kati ya mwaka 1995-2005, kimetangazwa na rais John Magufuli.
Aidha, Magufuli ametangaza siku saba za maombolezi, na katika kipindi hicho chote, bendera nchini humo zitapepea nusu mlingoti.
Mkapa, rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, atakumbukwa kwa juhudi zake za kusuluhisha migogoro ya kisiasa katika nchi jirani wakati alipokuwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
Baada ya machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka 2007, yeye pamoja na Hayati Koffi Annan aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Gracia Machel walisaidia upatikanaji wa maridhiano ya kisiasa nchini humo.
Aidha, alishiriki pakubwa sana katika mazungumzo ya amani ya kisiasa ya Burundi mwaka 2016 yaliyokuwa yanafanyika mjini Arusha.
Kifo chake kimetokea wakati taifa hilo linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.
Pamoja na mambo mengine, Watanzania watamkumbuka kwa kuhimiza wawekezaji kutoka nje kuja nchini humo kusaidia kuimarisha uchumi wa taifa hilo.