KENYA-CORONA-AFYA

Visa vipya 796 vyaripotiwa nchini Kenya

Afisa wa afya katika manispaa ya jiji la Nairobi akinyunyuzia dawa dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika soko kuu la Nairobi, Kenya, Mei 2, 2020.
Afisa wa afya katika manispaa ya jiji la Nairobi akinyunyuzia dawa dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika soko kuu la Nairobi, Kenya, Mei 2, 2020. REUTERS/Njeri Mwangi

Kenya imeripoti visa vipya 796 vya maambukizi ya Corona, ikiwa ndio idadi kubwa kuwahi kuripotiwa tangu kisa cha kwanza mwezi Machi mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Nchi hiyo sasa ina visa Elfu 15 na Mia Sita, huku jiji la Nairobi likiendelea kuwa na maambukizi makubwa.

Katibu Mkuu katika Wizara ya afya Daktari Mercy Mwanagangi ameonya kuwa maambukizi yanaendelea kuongezeka kwa sababu wanananchi wanakaidi kanuni za kujilinda, huku akionya kukithiri kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake katika kipindi hiki.

Wiki hii Wizara ya Afya nchini Kenya ilisema idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha kutokana na virusi vya Corona, wanasumbuliwa na shinikizo la damu, kisukari, saratani na virusi vya Ukimwi.

Siku ya Jumatatu wiki ijayo, rais Uhuru Kenyatta atakutana na Magavana kutathmini mwenendo wa maambukizi hayo baada ya kufunguliwa kwa mipaka ya Kaunti mbalimbali.

Hayo yanajiri wakati Shirika la Afya Duniani, WHO, na kituo cha udhibiti wa magonjwa barani Afrika, CDC, yameanzisha juhudi kuangalia uwezekano wa madawa ya mitishamba katika kupambana na janga la virusi vya Corona.