RWANDA-UFARANSA-HAKI

Uchunguzi dhidi ya afisa mwandamizi wa zamani wa Rwanda wafunguliwa Ufaransa

Picha za waathiriwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda katika eneo la ukumbusho la mauaji ya Kimbari huko Kigali.
Picha za waathiriwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda katika eneo la ukumbusho la mauaji ya Kimbari huko Kigali. REUTERS/Noor Khamis

Ofisi ya mashtaka dhidi ya ugaidi nchini Ufaransa imetangaza kufunguliwa kwa uchunguzi wa awali kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu dhidi ya afisa wa zamani wa Rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Uchunguzi wa awali ulifunguliwa Ijumaa Julai 24 kwa "uhalifu dhidi ya binadamu" dhidi ya Aloys Ntiwiragabo, mkuu wa idara ya ujasusi ya kijeshi, wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, ofisi ya mashitaka dhidi ya ugaidi ilisema Jumamosi Julai 25.

Uchunguzi huu ulifunguliwa kufuatia nakala iliyochapishwa siku ya Jumamosi na gazeti la Mediapart.

Tovuti hii ya habari inadai kwamba ilipata habari za Aloys Ntiwiragabo, 72, karibu na mji wa Orléans, kilomita mia moja kusini mwa mji wa Paris. Ofisi ya mashtaka dhidi ya ugaidi imebaini kwamba imeamua kushughulikia kesi hiyo baada tu ya kuchapishwa kwa nakala hiyo na kuwa imefungua uchunguzi wa awali kwa lengo la kuhakiki habari ya gazeti la Mediapart.

Ofisi ya mashtaka inabaini kuwa hadi leo hakuna malalamiko yoyote au hati ya waranti dhidi ya afisa huyo mwandamizi wa zamani wa Rwanda, iwe nchini Ufaransa, Rwanda au kutoka polisi ya kimataifa, Interpol.

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) ilitoa waranti wa kukamatwa dhidi yake mnamo mwaka 1998 na 2002, kisha kufutwa miaka kadhaa iliyopita. Katika mashtaka ya ICTR, Aloys Ntiwiragabo anatajwa kama sehemu ya kikundi cha maafisa ambao kati ya mwaka 1990 na 1994 "walikubaliana kupanga mpango kwa nia ya kuwaangamiza raia kutoka jamii ya Watutsi na wanasiasa wa upinzani na hivyo kubaki madarakani ”. Iilidaiwa pia kuwa kulikuwa kukitolewa kila mara orodha ya Watutsi na wapinzani ili "kuangalmizwa". Lakini waranti zote hizo za kukamatwa zilifutwa miaka kadhaa iliyopita.

Nchini Ufaransa, kulingana na upande wa mashtaka, kutajwa tu kwa jina lake kulianzia mwaka 2011 wakati mahakma ya kupambana na ugaidi ya Ufaransa ilipotaka kumsikiliza kama shahidi katika muktadha wa utaratibu uliolenga mmoja wa wasaidizi wake. Wakati huo, viongozi wa Rwanda walidai kwamba Aloys Ntiwiragabo alikuwa mafichoni katika moja ya nchi za Afrika.