KENYA-CORONA-AFYA

Idadi ya vifo vinavyohusiana na Corona yapindukia 299 nchini Kenya

Kenya imerekodi vifo 299 kutokana na virusi vya Corona baada ya vifo vipya 14 kuthibitishwa katika kipindi cha saa 24. Maafisa wanne wa Afya ni miongoni mwa wale waliofariki kutokana na virusi hivyo nchini humo.

Kenya inaendelea kuripoti visa zaidi vya maambukizi ya viriusi vya Corona.
Kenya inaendelea kuripoti visa zaidi vya maambukizi ya viriusi vya Corona. REUTERS/Jackson Njehia
Matangazo ya kibiashara

Idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona imefikia 18,581 baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza wagonjwa wengine 606.

Kati ya wagonjwa hao wapya 583 ni raia wa Kenya, huku 23 wakiwa raia wa kigeni, wanaume wakiwa 409 nao wanawake wakiwa 197, Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe amesema.

Mgonjwa mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa miezi minne, huku mtu mwenye umri mkubwa zaidi akiwa mzee wa miaka 85, Waziri wa Afya wa Kenya ameongeza.

Kufikia sasa Nairobi inaongoza kwa wagonjwa 448, ikifuatiwa na Kaunti ya Kajiado (25), Kaunti ya Machakos imerekodi visa vya maambukizi 16, Kaunti ya Uasin Gishu ina wagonjwa 11, Kaunti ya Nakuru ina wagonjwa 11, Kericho ina wagonjwa 9, Busia 7, Mombasa 7, Garissa 6, Bomet 3, Nyeri 2, Narok 2, Nandi 2, huku Kaunti za Embu, Lamu, Murang'a zikiwa na mgonjwa mmoja mmoja.

Waziri Kagwe amewataka wakazi wa eneo la Embakasi kuchukua tahadhari, huku akilitaja eneo hilo kuwa na wagonjwa wengi katika mji wa Nairobi.Wakati huo huo Waziri Mutahi Kagwe, amewataka raia wa Kenya kuheshimu kanuni za usafi, huku akiwatolea wito wa kutoruhusu wageni majumbani mwao ama hata kuzuru mashambani hadi iwapo kuna dharura.