TANZANIA-MKAPA-SIASA

Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa azikwa kijijini Lupaso-Masasi

Picha ya zamani inaonyesha Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa, Desemba 9, 2005, wakati wa sherehe ya maadhimisho ya miaka 44 ya uhuru wa Tanzania.
Picha ya zamani inaonyesha Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa, Desemba 9, 2005, wakati wa sherehe ya maadhimisho ya miaka 44 ya uhuru wa Tanzania. MWANZO MILLINGA / AFP

Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa mezikwa leo kijijini kwake Lupaso, kusini mwa Tanzania. Shughuli za mazishi zimehudhuriwa na mamia ya watu wakiongozwa na rais wa Tanzania John Pmbe Magufuli.

Matangazo ya kibiashara

Mkapa aliyeongoza Tanzania kati ya mwaka 1995-2005 alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo, familia yake ilielezea.

Baada ya ibada za kidini na risala za rambirambi, jeshi la Tanzania limetoa heshima za mwisho na kumzika amiri jeshi mkuu mstaafu Benjamin Mkapa kwa taratibu zao. Hayati Mkapa ameagwa kwa mizinga 21.

Alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania kuingia madarakani baada ya uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995.

Baada ya kumaliza utawala wake na rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005,bwana Mkapa alianzisha taasisi binafsi ambayo iliongoza mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi nchini humo.

Rais Mkapa katika utawala wake, alisifika kwa kauli mbiu ya uwazi na ukweli.

Mkapa, rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, atakumbukwa kwa juhudi zake za kusuluhisha migogoro ya kisiasa katika nchi jirani wakati alipokuwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

Baada ya machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka 2007, yeye pamoja na Hayati Koffi Annan aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Gracia Machel walisaidia upatikanaji wa maridhiano ya kisiasa nchini humo.

Aidha, alishiriki pakubwa sana katika mazungumzo ya amani ya kisiasa ya Burundi mwaka 2016 yaliyokuwa yanafanyika mjini Arusha.

Kifo chake kimetokea wakati taifa hilo linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.