TANZANIA-MKAPA-SIASA

Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa kuzikwa leo

Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa. UN Photo/JC McIlwaine

Rais wa mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa aliyefariki dunia wiki iliyopita anazikwa leo Jumatano mchana katika kijiji alikozaliwa cha Lupaso, katika Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, Kusini mwa Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya Watanzania walikusanyika jana Jumanne katika uwanja wa Uhuru kumwaga rais wao wa zamani.

Rais John Magufuli aliyewaongoza waombolezaji hao alimkumbuka mtangulizi wake kama mtu muhimu katika maisha yake, aliyemsaidia kwa mengi na wakati wa hotuba yake, alionekana kutoa machozi.

Tayari mwili wa Mkapa umewasili katika kijiji alichozaliwa kwa mazishi.

Mkapa aliyeongoza Tanzania kati ya mwaka 1995-2005 alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo.

Rais Mkapa katika utawala wake, alisifika kwa kauli mbiu ya uwazi na ukweli.

Mkapa, rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, atakumbukwa kwa juhudi zake za kusuluhisha migogoro ya kisiasa katika nchi jirani wakati alipokuwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

Baada ya machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Kenya mwaka 2007, yeye pamoja na Hayati Koffi Annan aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Gracia Machel walisaidia upatikanaji wa maridhiano ya kisiasa nchini humo.

Aidha, alishiriki pakubwa sana katika mazungumzo ya amani ya kisiasa ya Burundi mwaka 2016 yaliyokuwa yanafanyika mjini Arusha.

Kifo chake kimetokea wakati taifa hilo linapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.