TANZANIA-LISUU-CHADEMA-UCHAGUZI-SIASA

Lissu apitishwa na chama chake cha CHADEMA kuwania katika uchaguzi wa urais Tanzania

Baraza kuu la chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA limependekeza jina la mwanasiasa mkosoaji mkubwa wa serikali, Tundu Lissu kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Chama cha upinzania Tanzania CHADEMA champitisha TIndu Lissu kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa urais ujao.
Chama cha upinzania Tanzania CHADEMA champitisha TIndu Lissu kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa urais ujao. CHADEMA Tanzania/twitter.com
Matangazo ya kibiashara

Tundu Lissu ameshinda baada ya kujizolea kura 405 sawa na asilimia 91 ya kura 442 zilizopigwa, huku Lazaro Nyalandu akipata kura 36 wakati Dakta Maryrose Majige aliambulia kura moja.

Wakati huohuo Baraza Kuu la Chadema limempitisha Salum Mwalimu kuwa Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Naye Said Issa Mohammed amepitishwa na baraza hilo kuwa mgombea wa urais wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya matokeo hayo kutangazwa, Tundu Lissu Lissu amesema ushindi wake ni wa chama na kazi mbele yao bado ni ngumu.

Tundu Lissu pamoja na kukabiliwa na kesi sita za uchochezi bado anaamini kuwa kesi hizo haziwezi kuwa kikwazo kwa yeye kugombea urais na kwamba haitakuwa kazi rahisi kushindwa katika kesi hizo.

Jina la Tundu Lissu litawsilishwa katika mkutano mkuu wa chama cha CHADEMA ambao una mamlaka ya kumuidhinisha kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho cha upinzani nchini Tanzania.

Tindu Lissu alirejea nchini humo wiki iliyopita, akitokea nchini Ubelgiji alikokuwa anapata matibabu baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana karibu miaka mitatu iliyopita.

Chama kingine cha upinzani cha ACT Wazalendo kinatarajiwa kumtangaza mgombea wake siku ya Jumatano, huku aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya nje Bernard Membe, akitajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kupata tiketi hiyo.

Rais Magufuli anatetea kiti hicho kwa muhula wa pili kwa niaba ya chama tawala cha CCM.