KENYA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Maambukizi nchini Kenya yapindukia 23,202

Kenya inaendelea kuripoti visa zaidi vya maambukizi ya virusi vya Corona.
Kenya inaendelea kuripoti visa zaidi vya maambukizi ya virusi vya Corona. REUTERS/Baz Ratner

Kenya imeripoti visa vingine 605 vya maambukizi ya Corona na kufikisha idadi ya watu waliombukizwa tangu mwezi Machi kufikia zaidi ya Elfu 23 na 200.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na maambukizi hayo, idadi ya watu waliopona, inakaribia zaidi ya Elfu 10.

Wizara ya afya nchini Kenya inasema maambukizi yanaongezeka kwa sababu watu wengi nchini humo wanaendelea kukaidi maagizo ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya watu 388.

Hivi karibuni shirika la Afya Duniani WHO lilisema linahofia ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona barani Afrika, huku likionya kuwa kuendelea kushuhudiwa kwa ongezeko hilo hasa nchini Afrika Kusini, huenda hatua hiyo ikaathiri mataifa mengine barani Afrika.

Bara la Afrika limeshuhudia vifo vya watu Elfu 15 na wengine zaidi ya Laki Saba na Elfu 25, wamemabukizwa virusi vya janga hilo hatari.

Kufikia sasa ugonjwa wa Covid-19 umesababisha vifo vya watu 692,000 duniani baada ya vifo vipya 4,3 10 kuthibitishwa, huku visa Milioni 18.4 vya maambukizi vikiripotiwa, baada ya visa vipya laki 2 na Elfu 24 vya maambukizi kuthibitishwa. Wagonjwa Milioni 11 wakithibitishwa kupona ugonjwa huo.

Hayo yanajiri wakati China na Shirika la Afya Duniani, WHO, zinajadili mipango ya kubaini chanzo cha mripuko wa virusi vya corona, kufuatia ziara nchini humo, ya wataalamu wawili wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Virusi vya Corona vilibainika kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan katikati mwa China, mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, na vimehusishwa na soko la jumla la vyakula, ambako wanyama wa porini wanauzwa.