Kenya: KEMRI yarekebisha idadi ya Wakenya walioambukizwa Covid-19
Utafiti kutoka taasisi ya uchunguzi wa Tiba nchini Kenya KEMRI sasa unaonesha kuwa, huenda Wakenya Milioni 1.6 waliambukizwa virusi vya Corona na kujijengea kinga badala ya Milioni 2.7 idadi iliyokuwa imetangazwa mwezi Aprili.
Imechapishwa:
Taasisi hiyo inasema, imebaini hilo baada ya utafiti wa kina kwa sampuli ya damu iliyotolewa na Wakenya wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64.
Utafiti huu umekuja wakati huu nchi hiyo ikiripoti maambukizi mapya 538 ya virusi hivyo.
Mapema wiki hii watu 48 kutoka famila moja katika Kaunti ya Migori, waliambukizwa virusi vya Corona kutoka kwa mwanafamilia mmoja aliyekuwa amesafiri kutoka jijini Nairobi, huku nchini hiyo ikiendelea kuripoti maambukizi zaidi.
Hayo yanajiri wakati China na Shirika la Afya Duniani, WHO, zinajadili mipango ya kubaini chanzo cha mripuko wa virusi vya corona, kufuatia ziara nchini humo, ya wataalamu wawili wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
Virusi vya Corona vilibainika kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan katikati mwa China, mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, na vimehusishwa na soko la jumla la vyakula, ambako wanyama wa porini wanauzwa.
Hivi karibuni shirika la Afya Duniani, WHO, liliaonya kuwa licha ya jitihada zinazofanyika kutafuta chanjo na dawa ya kupambana na janga la virusi vya Corona, huenda kusiwe na suluhu ya muda mrefu ya kukabiliana na janga hili.