TANZANIA-SIASA-USALAMA

Serikali ya Tanzania yaonya vyama vya siasa vitakavyochochea vurugu kuelekea uchaguzi

Sehemu ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililoko mjini Dodoma, makao makuu ya nchi.
Sehemu ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililoko mjini Dodoma, makao makuu ya nchi. Ikulu/Tanzania

Waziri wa Mambo ya ndani nchini Tanzania, George Simbachawene amevionya vyama vya siasa, anavyosema vinafanya siasa zenye viashiriia vya kuzusha vurugu, na sasa anataka vyombo vya usalama kuvidhbuti bila kujali chama.

Matangazo ya kibiashara

Aidha, ameonya kuwa kuelekea Uchaguzi Mkuu tarehe 28 mwezi Oktoba, wanasiasa wanaohamasisha vurugu hawatavumiliwa.

Haya yanajiri wakati hivi karibuni Watu wasiojulikana walidiwa kuvamia na kuchoma moto jengo la ofisi ya chama kikuu cha upinzani cha Chadema katika kata ya Kimandolu tarafa ya Suye katika halmashauri ya jiji la Arusha, na kusababisha uharibifu wa mali ambazo thamani yake haijajulikana.

Kwa sasa vyama vya siasa nchini Tanzania vinajianda kuanza kampeni za uchaguzi mkuu wa urais,ubunge, udiwani ifikapo Agosti 26 mwaka huu wa 2020 ambapo uzinduzi utafanyika kwa vyama mbalimbali na kudumu kwa takribani siku 60, huku dalili zikionesha kutakuwa na ushindani mkali katika nafasi ya urais ambapo jumla vyama vya siasa 16 vimeweka wagombea wao kufikia sasa.

Kampeni hizo zitamalizika tarehe ya uchaguzi mkuu Oktoba 28 ambapo mamilioni ya Watanzania watapiga kura kuchagua viongozi wapya watakaopokea kijiti cha uongozi cha miaka mitano ijayo. Huu ni uchaguzi wa sita tangu nchi hiyo iliporejea kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Mabadiliko ya upashanaji habari na matumizi makubwa ya mitandao, ukosefu wa ajira, ghadhabu za kunyimwa fursa ya mikutano ya hadhara, hali ya uchumi, haki za binadamu, miradi mikubwa ya maendeleo, uhuru wa tume ya uchaguzi, kuibuka hamasa ya kisiasa miongoni mwa wananchi pamoja na ajenda ya usalama wa raia na viongozi wao ni baadhi ya mambo yanayotarajiwa kutawala sehemu kubwa ya kampeni za uchaguzi huo.