KENYA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Idadi ya vifo yapindukia zaidi ya 500 Kenya

Wakazi wa eneo la Kibera jijini Nairobi wanarudi nyumbani kabla ya muda uliowekwa wa kutotembea kuanza katika kubambana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona Machi 27, 2020.
Wakazi wa eneo la Kibera jijini Nairobi wanarudi nyumbani kabla ya muda uliowekwa wa kutotembea kuanza katika kubambana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona Machi 27, 2020. REUTERS/Thomas Mukoya

Kenya imeripoti vifo 19 vinavyotokana na maambukizi ya Corona, na kufikisha idadi ya watu waliopoteza maisha tangu kuzuka kwa janga hilo nchini kufikia 506.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo, watu wengine 379 wameambukizwa virusi hivyo ndani ya saa 24 zilizopita.

Wizara ya afya nchini Kenya inaonya kuwa pamoja na idadi ya maambukizi kuanza kushuka ni mapema kusema iwapo nchi hiyo inaelekea kushinda vita dhidi ya janga hilo.

Wiki hii Wizara ya afya nchini Kenya ilikanusha ripoti za ubadhirifu mkubwa wa fedha za wahisani zilizotolewa kukabiliana na janga la Corona, linaloendelea kuiathiri nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.

Kituo cha Televisheni cha NTV kilitoa ripoti ya uchunguzi iliyoonesha kuwa zaidi ya Dola za Marekani Milioni 400 hazijulikani zilivyotumika.

Hivi karibuni shirika la Afya Duniani, WHO lilisema bara la Afrika litaendelea kushuhudia ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona wakati huu nchi nyingi zinapoanza kufungua mipaka yake na maisha kuanza kurejea taratibu, katika bara hilo ambalo lina maambukizi zaidi ya Milioni Moja.

WHO pia lilisema linahofia ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona barani Afrika, huku likionya kuwa kuendelea kushuhudiwa kwa ongezeko hilo hasa nchini Afrika Kusini, huenda hatua hiyo ikaathiri mataifa mengine barani Afrika.