UFARANSA-RWANDA-KABUGA-HAKI

Rufaa ya Félicien Kabuga, mshukiwa mkuu wa mauaji ya kimbari kuchunguzwa Septemba 2 Paris

Félicien Kabuga, anayeshtumiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa katuni akiwa mahakamani Mei 20, 2020.
Félicien Kabuga, anayeshtumiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa katuni akiwa mahakamani Mei 20, 2020. Benoit PEYRUCQ / AFP

Mahakama ya juu nchini Ufaransa itachunguza rufaa iliyowasilishwa na Félicien Kabuga, mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Septemba 2.

Matangazo ya kibiashara

Félicien Kabuga aliwasilisha rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya paris kuhusu kupekekwa katika mahakama ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Rwanda-'International Residual Mechanism for Criminal Tribunals' (IRMCT) mjini Hague - mahakama inayosikiliza kesi za uhalifu wa vita za Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia.

Hata hivyo Félicien Kabuga na familia yake bado wana imani kuwa uamuzi huo utafutwa. Félicien Kabuga anayetuhumiwa kuwa 'mfadhili mkuu' wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari alikamatwa huko Asnières-Sur-Seine, karibu na mji wa Paris Mei 16 eneo ambalo alikuwa anaishi kwa kutumia majina bandia, baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 25.

Marekani ilitoa dau la dola milioni 5 kwa atakayeweza kutoa taarifa kuhusu bwana Kabuga ili aweze kukamatwa.

Mahakama ya kimataifa ya mauji ya kimbari yaliyotokea Rwanda ilimshtaki bwana Kabuga mwenye umri wa miaka 84 kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Anadaiwa kuwa mfadhili mkuu wa Wahutu wenye itikadi kali ambao waliuwa watu 800,000 mwaka 1994.

Walikuwa wanawalenga kundi dogo la watu wachche kutoka jamii ya Watutsi pamoja na wapinzani wao siasa, hasa kutoka jamii ya Wahutu.

Félicien Kabuga ni mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, ambaye alichukuliwa kuwa mtu tajiri zaidi nchini humo kabla ya kufanyika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Alizaliwa katika eneo la kaskazini mwa Rwanda ambako alijilimbikizia mali kutokana na biasahara ya majani ya chai miaka ya 1970 na kuwekeza katika biashara tofauti nchini humo, mataifa jirani na ng'ambo.

Alikuwa mwandani wa karibu wa chama tawala cha MRND na baba mkwe wa rais Juvénal Habyarimana.

Kabuga anayetuhumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari , alikuwa mwenye hisa mkuu katika kituo cha radio ya kibinafsi RTLM ambacho kililaumiwa kwa kuwahamasisha watu wa jamii ya Kihutu kuwaua wenzao wa Watutsi.

Kutokana na utajiri wake, baada ya mauaji ya kimbari Kabuga, mwenye umri wa miaka 84, alifanikiwa kujificha katika mataifa mengi hadi alipokamatwa Mei 16,2020.