RWANDA-UFARANSA-MEDIAPART-HAKI

Mauaji ya kimbari ya Rwanda: Kigali yatoa waranti dhidi ya Aloys Ntiwiragabo

Mnyarwanda huyu anasoma taarifa iliyochapishwa na TV5 kuhusu Aloys Ntiwiragabo.
Mnyarwanda huyu anasoma taarifa iliyochapishwa na TV5 kuhusu Aloys Ntiwiragabo. AFP

Aloys Ntiwiragabo, Mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi wa jeshi nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994 anatafutwa ili kujibu mashitaka yanayomkabili, baada ya Rwanda kutoa waranti wa kimataifa wa kukamatwa dhidi yake Jumanne Agosti 25.

Matangazo ya kibiashara

Aloys Ntiwiragabo pia anatafutwa na Ufaransa kwa uchunguzi zaidi tangu mwishoni mwa mwezi Julai kufuatia nakala iliyochapishwa na Gazeti la Mediapart.

Wakati huo ofisi ya mashtaka dhidi ya ugaidi nchini Ufaransa ilitangaza kufunguliwa kwa uchunguzi wa awali kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu dhidi ya Aloys Ntiwiragabo.

Tovuti hii ya habari inadai kwamba ilipata habari za kuepo kwa Aloys Ntiwiragabo, 72, karibu na mji wa Orléans, kilomita mia moja kusini mwa mji wa Paris.

Kulingana na wakili wake aliyehojiwa na RFI, Aloys Ntiwiragabo hajifichi. Lakini baadhi ya waathirika wa mauaji ya kimbari wana hofu kwamba anaweza kutoweka tena. Ombi la Kigali linaweza kusaidia kuharakisha utaratibu wa kisheria.

Hivi karibuni mwanasheria wake Benjamin Chouai, alidai kuwa habari za Gazeti la Mediapart ni za uongo na alibaini kwamba mteja wake yuko tayari kujibu maswali yoyote ya mahakama ya Ufaransa.

Ofisi ya mashtaka dhidi ya ugaidi ilibaini kwamba imeamua kushughulikia kesi hiyo baada tu ya kuchapishwa kwa nakala hiyo na kuwa imefungua uchunguzi wa awali kwa lengo la kuhakiki habari ya gazeti la Mediapart.

Awali Ofisi ya mashtaka ilibaini kuwa hakuna malalamiko yoyote au hati ya waranti dhidi ya afisa huyo mwandamizi wa zamani wa Rwanda, iwe nchini Ufaransa, Rwanda au kutoka polisi ya kimataifa, Interpol.

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) ilitoa waranti wa kukamatwa dhidi yake mnamo mwaka 1998 na 2002, kisha kufutwa miaka kadhaa iliyopita. Katika mashtaka ya ICTR, Aloys Ntiwiragabo anatajwa kama sehemu ya kikundi cha maafisa ambao kati ya mwaka 1990 na 1994 "walikubaliana kupanga mpango kwa nia ya kuwaangamiza raia kutoka jamii ya Watutsi na wanasiasa wa upinzani na hivyo kubaki madarakani ”. Iilidaiwa pia kuwa kulikuwa kukitolewa kila mara orodha ya Watutsi na wapinzani ili "kuangalmizwa". Lakini waranti zote hizo za kukamatwa zilifutwa miaka kadhaa iliyopita.

Nchini Ufaransa, kulingana na upande wa mashtaka, kutajwa tu kwa jina lake kulianzia mwaka 2011 wakati mahakma ya kupambana na ugaidi ya Ufaransa ilipotaka kumsikiliza kama shahidi katika muktadha wa utaratibu uliolenga mmoja wa wasaidizi wake. Wakati huo, viongozi wa Rwanda walidai kwamba Aloys Ntiwiragabo alikuwa mafichoni katika moja ya nchi za Afrika.