RWANDA-UFARANSA-HAKI

Mauaji ya kimbari nchini Rwanda: Hatma ya Félicien Kabuga kujulikana Septemba 30

Félicien Kabuga, anashukiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa mfano wa katuni akiwa mbele ya mahakama Mei 20, 2020.
Félicien Kabuga, anashukiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa mfano wa katuni akiwa mbele ya mahakama Mei 20, 2020. Benoit PEYRUCQ / AFP

Septemba 30, Mahakama Kuu ya Paris itatoa uamuzi wake ikiwa itathibitisha au la uamuzi uliochukuliwa mwezi Juni na mahakama ya Rufaa ya Ufaransa kumkabidhi Felicien Kabuga kwa mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda iliyopo mjini Arusha, nchini Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Félicien Kabuga anachukuliwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.

Jumanne, Septemba 2, kila upande uliwasilisha hoja zake. Suala ambalo limezua mijadala ni kuhusu hali ya afya ya Félicien Kabuga ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 88.

Wakili wa Félicien Kabuga anajaribu kuonyesha kwamba sheria ya Ufaransa kuhusu utekelezaji wa waranti wa kimataifa wa kukamatwa haielezi uchunguzi wa kina wa suala hili na kwa hivyo inakiuka kanuni ya msingi ya haki ya afya inayotolewa na Katiba. Anadai kuwa mteja wake anasumbuliwa na shinikizo la damu, lakini pia ugonjwa wa kisukari na leucoaraiosis, ugonjwa unaoathiri mishipa ya fahamu. Wakili huyo amesema kuwa uchunguzi kamili wa kitabibu ungelipaswa kufanywa kabla ya kuchukuliwa uamuzi wa kumkabidhi kwa mahakama ya Arusha.

Hoja hizo zimenpigwa na mwanasheria mkuu wa serikali, ambaye anadai kuwa Mahakama ya Rufaa iliheshimu kanuni za sheria, ikizingatia hasa cheti cha matibabu, kilichotolewa na idara ya afya katika gereza, ambayo ilibaini kwamba hali yake inaendana na mazingira ya kizuizini aliyomo. Amekumbusha pia kuwa Ufaransa inahusiana na azimio la Umoja wa Mataifa linalounda mahakama ya Arusha ambayo ynataka kumhukumu na kwamba kukataa kumkabidhi kwa mahakama hiyo kutachukuliwa kama kukataa ushirikiano.

Félicien Kabuga anayetuhumiwa kuwa 'mfadhili mkuu' wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari alikamatwa huko Asnières-Sur-Seine, karibu na mji wa Paris Mei 16 eneo ambalo alikuwa anaishi kwa kutumia majina bandia, baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 25.

Marekani ilitoa dau la dola milioni 5 kwa atakayeweza kutoa taarifa kuhusu bwana Kabuga ili aweze kukamatwa.

Félicien Kabuga ni mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, ambaye alichukuliwa kuwa mtu tajiri zaidi nchini humo kabla ya kufanyika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Alizaliwa katika eneo la kaskazini mwa Rwanda ambako alijilimbikizia mali kutokana na biasahara ya majani ya chai miaka ya 1970 na kuwekeza katika biashara tofauti nchini humo, mataifa jirani na ng'ambo.

Alikuwa mwandani wa karibu wa chama tawala cha MRND na baba mkwe wa rais Juvénal Habyarimana.

Kabuga anayetuhumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari , alikuwa mwenye hisa mkuu katika kituo cha radio ya kibinafsi RTLM ambacho kililaumiwa kwa kuwahamasisha watu wa jamii ya Kihutu kuwaua wenzao wa Watutsi.