BURUNDI-USALAMA

Burundi: Watatu wauawa karibu na mji mkuu Bujumbura

Mnara wa umoja wa Warundi, Bujumbura.
Mnara wa umoja wa Warundi, Bujumbura. Tourisme.gov.bi

Watu watatu, akiwemo kiongozi wa vijana kutoka chama tawala cha Cndd-Fdd wameuawa katika kijiji cha Maramvya, mkoani Rumonge, nchini Burundi baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha, ambao mwisho wa mwezi Agosti, 18 waliuawa katika makabiliano na maafisa wa usalama.

Matangazo ya kibiashara

Watu hao wenye silaha wanaaminiwa kujificha Milimani karibu na jiji kuu Bujumbura na wanadaiwa kuingia  nchini humo kupitia Ziwa Tanganyika, wakitokea Mashariki mwa DRC.

Licha ya viongozi kupuuzia mashambulio hayo wakisema, ni makundi ya wahalifu au ya wezi, kwa upande wa raia, wanahofia maisha yao.

Wana wasiwasi kuwa, huenda mashambulizi kama haya, yakasababisha machafuko nchini Burundi.

"Tuliisha sikia kwamba huko kwenye milima askari wanazidi kuwasaka watu hao. Tuna uoga, ukiwasikia watu hao ambao tulikua tumeisha wasahau, ni jambo la kutuvunja moyo, " mmoja wa wakazi amesema.

"Tuna uoga, lakini kwa kweli mimi sikuwaona, usingizi ni nusu kufa. Ilikuwa ni usiku, tuliwasikia wameisha panda huko kwenye milima. Sikuwaona na macho yangu. Nina presha, nikiwaona tu, ni kuarifu viongozi. Tunawaomba watutumie askari ili walinde usalama wetu sisi tunapoishi katika maeneo haya wanapopitia, " amesema mkaazi mwengine.

Spika wa bunge la Seneti Emmanuel Sinzohagera, anawaomba raia wanaoisha katika maeneo kunakoripotiwa makundi hayo yenye silaha kushirikiana na vikosi vya kulinda usalama.

"Yaliyopitika ni kama kututoa usingizini, uchaguzi ulimalizika, baadhi yetu tulikuwa baado tukisherehekea ushindi, na tukasinzia, kuna ulazima tuimarishe kamati za usalama, " amesema Emmanuel Sinzohagera.

Shambuulizi hili limekuja miezi mitatu baada ya Uchaguzi Mkuu kupelekea ushindi wa chama tawala cha Cndd-Fdd kinachoongozwa na rais Évariste Ndayishimiye.