SUDANI KUSINI-UN-USALAMA

Umoja wa Mataifa waanza kuondoka askari wake katika kambi 17 za wakimbizi Sudan Kusini

Mkimbizi akiandamana na askari wa kulinda amani, karibu na kambi ya kulinda raia (POC) ya Umoja wa Mataifa mjini Juba, Oktoba 4, 2016.
Mkimbizi akiandamana na askari wa kulinda amani, karibu na kambi ya kulinda raia (POC) ya Umoja wa Mataifa mjini Juba, Oktoba 4, 2016. ALBERT GONZALEZ FARRAN / AFP

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wameanza kuondoka kwenye kambi 17 za wakimbizi wa ndani nchini Sudan Kusini, ambazo wamekuwa wakitoa ulinzi kwa maelfu ya wakimbizi kwa muda wa miaka Saba.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii ya Umoja wa Mataifa haijapokelewa vema na mamia ya wakimbizi ambao wanaishi kwenye kambi hizo, ambapo wanadai kushtushwa.

“Wanajeshi hao wa umoja wa Mataifa waliondoka usiku. Hawakutujulisha kwamba wanaondoka” , mmoja wa wakimbizi amesema.

“Wakimbizi wamekuwa wakitoka kwenye sehemu moja hadi nyingine ya kambi wakiwa na hofu kubwa” ameongeza mkimbizi huyo.

Meja-Jenerali Joseph Akon, kamishina wa mojawapo ya majimbo kumi ambako wakimbizi wa ndani wamekuwa wakilindwa, amesema hakupewa taarifa rasmi ya kuondolewa kwa wanajeshi hao.

“Sijaarifiwa rasmi kwamba wanajeshi wa Umoja wa Mtaifa wanaondoka. Nilichoambiwa na Umoja wa Mataifa ni kwamba kuna mpango wa kuwapa makao mapya, “ Meja-Jenerali Joseph Akon amesema.

Licha ya wanajeshi hao kuondolewa, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer, amesema hakuna tishio kubwa la usalama tofauti na ilivyokuwa awali, akiwatoa hofu raia hao.

“Hakuna mkimbizi ambaye atalazimishwa kutoka kwenye kambi za wakimbizi wakati wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanapoondoka. Utoaji wa misaada kwa wakimbizi utaendelea. Kilichoko ni kwamba hatutahusika tena na kambi za wakimbizi. Litakuwa jukumu la serikali kuwatafutia makao wakimbizi ama iwasaidie kurudi makwao ambako nyumba zao sasa zinakaliwa na watu wengine, “ amesema David Shearer.

Kuondolewa kwa wanajeshi hawa kunakuja ikiwa ni miezi saba tu imepita tangu rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir na mpinzani wake, Riek Machar, kusaini mkataba wa amani.