UGANDA-MAWASILIANO-VYOMBO VYA HABARI

Serikali ya Uganda yatoa kanuni kudhibiti zaidi maudhui mtandaoni

Kiongozi wa upinzani Uganda Robert Kyangulanyi, akijulikana kwa jina maarufu Bobi Wine alipowasili kwenye makao ya chama chake kipya, National Unity Platform (NUP), wakati wa kuteuliwa kwake kama rais kiongozi wa chama hicho, Agosti 21, 2020.
Kiongozi wa upinzani Uganda Robert Kyangulanyi, akijulikana kwa jina maarufu Bobi Wine alipowasili kwenye makao ya chama chake kipya, National Unity Platform (NUP), wakati wa kuteuliwa kwake kama rais kiongozi wa chama hicho, Agosti 21, 2020. SUMY SADURNI / AFP

Tume ya Mawasiliano ya Uganda ilitangaza wiki iliyopita: kuanzia sasa, mtu yeyote anayechapisha mauadhui mtandaoni atalazimika kujiandikisha kabla ya Oktoba 5.

Matangazo ya kibiashara

Kwa kutetea azimio hili jipya, Tume ya Mawasiliano ya Uganda inataja kifungu cha mamlaka ya Sheria ya Mawasiliano ya Uganda (Uganda Communication Act), ambayo inapiga marufuku uchapishaji wa maudhui bila kibali. Sheria ambayo itatumika kwa machapisho ya maudhui mtandaoni na kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa upande wa Roland Ebole, mmoja wa watafiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Amnesty International kuhusu Uganda, amesema hiki ni kizuizi kingine kikubwa kuhusu uhuru wa kujieleza nchini. Kulingana na Roland Ebole, hatua hiyo inatia wasiwasi zaidi ikiwa imesalia miezi michache tu kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao.

"Kwa jumla, Waganda wote watalazimika kufuta kanuni hii mpya," amebaini Roland Ebole akihojiwa na Lucie Mouillaud, wa kitengo cha RFI katika kanda ya Afrika (RFI-Afrique). Tunapaswa kutambua kuwa uchaguzi wa rais unakaribia. Ikumbukwe pia kwamba mwanzoni mwa mwaka huu, mwezi Juni, tume ya uchaguzi ilitoa maagizo mapya, ambayo ni kama muongozo uliorekebishwa kwa uchaguzi wa mwaka 2021, na ambao unataka mchakato mzima wa uchaguzi ufanyike mtandaoni".

Lengo: kuzuia upinzani

Kama matokeo, ameongeza mtafiti wa Amnesty: "Mikusanyiko yote ya kisiasa wakati wa kampeni ni marufuku, kwa hivyo wakati kuna vizuizi kuhusu njia za mawasiliano na habari, wakati ambapo serikali inakataza mikusanyiko ya umma, tunaweza fikiria kuwa lengo la mchakato huu ni kuzuia upinzani. "