KENYA-KEMSA-CORONA-AFYA

KEMSA yashtumiwa matumizi mabaya ya fedha katika mapambano dhidi ya Corona Kenya

Afisa wa afya katika manispaa ya jiji la Nairobi akinyunyuzia dawa dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika katika soko kuu la Nairobi, Kenya, Aprili 19, 2020.
Afisa wa afya katika manispaa ya jiji la Nairobi akinyunyuzia dawa dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika katika soko kuu la Nairobi, Kenya, Aprili 19, 2020. REUTERS/Njeri Mwangi

Tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya imewasilisha ushahidi katika bunge la Senate unaonesha namna shirika la usambasaji dawa nchini humo KEMSA lilivyohusika kwenye sakata ya ufujaji wa Mabilioni ya fedha za kununua vifaa vya kupambana na janga la Corona.

Matangazo ya kibiashara

Tume hiyo iliyokabidhi ripoti yake kwa mkurugenzi wa mashataka nchini Noordin Haji mwishoni mwa wiki iliyopita, ilianza uchunguzi wake baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuamuru matumizi ya pesa za kupambana na janga la Corona kuchunguzwa kufuatia malalamiko kutoka kwa umma.

Katika ripoti yake ambayo ilikabidhiwa bunge la Senate, EACC imesema KEMSA imeshindwa kueleza kwa ushahidi tosha, namna shilingi bilioni saba nukta nane zilizovyotumika.

Aidha maafisa wa ngazi za juu katika shirika hilo wamebainika kuhusika kwenye ununuzi wa vifaa vya kimatibabu kwa gharama ya juu  na ukiukaji mkubwa wa sheria za ununuzi wa serikali.

Katika ripoti nyingine ya mamlaka ya kutathmini manunuzi ya serikali, KEMSA inadaiwa kununua kwa mfano dawa za Paracetemol na vitakasa mkono kwa bei iliyo juu mara mbili ,wakati huu wa janga la Corona.

Ripoti hiyo inajiri wakati Kenya ikiwa imeshuhudia migomo ya kila mara ya wafanyakazi katika sekta ya afya wakilalamikia kukosa vifaa maalum vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Corona wanapokuwa kazini.

Kamati ya pamoja kutoka bunge la kitaifa na lile la Senate bado wanaendelea kufanya uchunguzi wao kuhusu sakata hiyo.