BURUNDI-EU-USHIRIKIANO

Burundi: Ndayishimiye ainyooshea kidolea cha lawama EU "kuhusika" katika jaribio la mapinduzi la 2015

Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, Juni 26, 2020 katika uwanja wa Ingoma huko Gitega.
Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, Juni 26, 2020 katika uwanja wa Ingoma huko Gitega. AFP Photos/Tchandrou Nitanga

Wakati wa mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu kuapishwa kwake, rais wa Burundi, Jenerali Évariste Ndayishimiye, ameshambulia kwa maeneo makali Umoja wa Ulaya na kuushutumu kushiriki katika jaribio la mapinduzi la mwaka 2015.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo Jenerali Ndayishimiye amebaini kwamba Burundi na Umoja huo wanataka kuanzisha upya mazungumzo.

Kwa muda wa saa tatu, rais wa Burundi alijibu maswali ya waandishi wa habari, kipindi ambacho kilirushwa hewani kwenye vyombo vyote vya habari vya serikali na vya kibinafsi nchini humo. Ulikuwa mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu kuapishwa kwake, zaidi ya miezi mitatu iliyopita.

Wakati wa mkutano huu na vyombo vya habari, hotuba ya Jenerali Évariste Ndayshimiye kuhusu Umoja wa Ulaya ilikuwa moja ya mada kuu na muhimu. Burundi iko tayari kufufua uhusiano na Jumuiya ya Ulaya, lakini sio kwa masharti, alisema Ndayishimiye, akiishutumu moja kwa moja Umoja huo kwa kushiriki katika jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 dhidi ya mtangulizi wake, hayati Pierre Nkurunziza.

'Kila jambo lina mwisho wake'

"Uhusiano wetu na Umoja wa Ulaya ulizorota kwa sababu tuligundua kuwa moja huo ulihusika katika jaribio la mapinduzi la mwaka 2015. Kwa kuwa hawakuweza kutushinda kwa kutumia nguvu, walisema: "Wacha tuchukue vikwazo dhidi ya serikali hii ili umaskini uiangushe", kwa bahati nzuri Mungu yuko pamoja nasi, ametusaidia", alisema.

Umoja wa Ulaya ndio mfadhili mkubwa wa Burundi ambao uliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya serikali ya Gitega tangu mwaka 2016, wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa kutokana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya serikali.

Baada ya hapo, rais wa Burundi alisema yuko wazi kuanzisha mazungumzo hayo. "Kila jambo lina mwisho wake. Hii ndio sababu leo, tayari tumewatangazia: "Hatukuwafukuza, mliondoka wenyewe. Ikiwa mnataka kurejesha uhusiano (nasi), mlango uko wazi", "alisema. mbele ya waandishi wa habari kabla ya kuongeza kuwa "jambo muhimu zaidi kwetu ni kwamba Burundi iko wazi kwa ushirikiano".

"Ikiwa wanataka tushirikiane kweli, hakuna shida kwa sababu hatujawahi kusema kwamba tumechukua vikwazo dhidi ya Umoja wa Ulaya. Lakini kuchukua azimio hili ama lile, sio jambo sahihi, lazima uwe na mazungumzo. Tunajua kwamba Mkataba wa Cotonou una maana yake, na kwamba tuko katika mchakato wa kuujadili, tunaendelea kusonga mbele, "alihitimisha.

Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia, Gitega na Brussels wako katika harakati za kuanza tena mazungumzo ya kisiasa yaliyokwama kwa miaka mitano. Umoja wa Ulaya umesema uko tayari kushirikiana na utawala mpya wa Burundi, lakini utaomba Gitega kuonyesha "baadhi ya ishara", ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa waandishi wa habari na mwanaharakati nayezuiliwa jela.