KENYA-CORONA-AFYA

Coronavirus: Rais wa Kenya aongeza muda wa masharti kwa siku 60

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amebaini kwamba shule hazitafunguliwa hadi usalama wa wanafunzi uzingatiwe.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amebaini kwamba shule hazitafunguliwa hadi usalama wa wanafunzi uzingatiwe. Yasuyoshi CHIBA / AFP

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kuongeza muda wa wa masharti kwa siku nyingine sitini katika kukabiliana na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa COVID-19 nchini Kenya, huku akibaini kwamba masharti ya kutotoka majumbani sasa yataanza kutekelezwa saa tano usiku (badala ya saa tatu usiku) hadi saa kumi alfajiri.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo Rais Kenyatta amebaini kwamba shule hazitafunguliwa hadi usalama wa wanafunzi uzingatiwe. Ameyasema hayo kwenye kongamano la kitaifa kuhusu janga la COVID-19.

Kufikia leo Jumatatu, Virusi vya Corona vimewaathiri watu 38,115, huku wagonjwa 24,621 wakithibitishwa kupona ugonjwa huo hatari na 691 wamefariki duniania.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi nchini humo wanaona kuwa, huu ni wakati wa uchumi wa nchi hiyo kufunguliwa tena baada ya wizara ya afya kusema kuwa maambukizi yamepungua.

Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa COVID-19, ulitokea katika mkoa wa Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.

Kufikia sasa kinachojulikana ni kuwa Covid-19, ni ugonjwa ambao unaothiri mfumo wa kupumua wa binadamu.

Dalili zake ni pamoja na homa kali, kukohoa ambako baada ya wiki moja muathiriwa anakabiliwa na tatizo la kupumua.