UFARANSA-RWANDA-KABUGA-HAKI

Hatma ya Félicien Kabuga kujulikana Jumatano wiki hii

Félicien Kabuga, anashukiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa mfano wa katuni akiwa mbele ya mahakama Mei 20, 2020.
Félicien Kabuga, anashukiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa mfano wa katuni akiwa mbele ya mahakama Mei 20, 2020. Benoit PEYRUCQ / AFP

Mahakama ya Rufaa nchini Ufaransa siku ya Jumatano  inatarajiwa kutoa uamuzi iwapo Felicien Kabuga anayedaiwa kufadhili mauaji ya kimbari nchini Rwanda, atashtakiwa nchini Ufaransa au katika mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda iliyopo mjini Arusha, nchini Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Kabuga alikamatwa mwezi Mei nyumani kwake jijini Paris baada ya kutafutwa kwa miaka 25, na anakabiliwa na mashtaka ya makosa ya kuyafadhili makundi yenye silaha wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka wa 1994 ambayo yalisababisha vifo vya wato laki nane ikiwa ni pamoja na Watutsi na Wahutu wenye msimamo wastani.

Félicien Kabuga anayetuhumiwa kuwa 'mfadhili mkuu' wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari alikamatwa huko Asnières-Sur-Seine, karibu na mji wa Paris Mei 16 eneo ambalo alikuwa anaishi kwa kutumia majina bandia, baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 25.

Marekani ilitoa dau la dola milioni 5 kwa atakayeweza kutoa taarifa kuhusu bwana Kabuga ili aweze kukamatwa.

Félicien Kabuga ni mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, ambaye alichukuliwa kuwa mtu tajiri zaidi nchini humo kabla ya kufanyika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Alizaliwa katika eneo la kaskazini mwa Rwanda ambako alijilimbikizia mali kutokana na biasahara ya majani ya chai miaka ya 1970 na kuwekeza katika biashara tofauti nchini humo, mataifa jirani na ng'ambo.

Alikuwa mwandani wa karibu wa chama tawala cha MRND na baba mkwe wa rais Juvénal Habyarimana.

Kabuga anayetuhumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari , alikuwa mwenye hisa mkuu katika kituo cha radio ya kibinafsi RTLM ambacho kililaumiwa kwa kuwahamasisha watu wa jamii ya Kihutu kuwaua wenzao wa Watutsi.