RWANDA-UFARANSA-ICC-KABUGA-HAKI

Félicien Kabuga kukabidhiwa Mahakama ya kimataifa

Félicien Kabuga, anashukiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa mfano wa katuni akiwa mbele ya mahakama Mei 20, 2020.
Félicien Kabuga, anashukiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, hapa akioneshwa kwa mfano wa katuni akiwa mbele ya mahakama Mei 20, 2020. Benoit PEYRUCQ / AFP

Mahakama ya Juu jijini Paris nchini Ufaransa imethibitisha Jumatano hii, Septemba 30 uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wa kumkabidhi, Félicien Kabuga kwa mahakama ya kimataifa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa hivyo Ufaransa sasa ina muda wa mwezi mmoja kumkabidhi Félicien Kabuga kwa mahakama ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Rwanda-'International Residual Mechanism for Criminal Tribunals' (IRMCT) mjini Hague - mahakama inayosikiliza kesi za uhalifu wa vita za Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia.

Kitengo cha Mahakama ya Juu hatimaye kimefutilia mbali rufaa iliyoletwa na mawakili wa Félicien Kabuga kuzuia asikabidhiwe mahakama ya kimataifa. K

Mwezi Juni Mahakama ya Rufaa ya Paris iliamua Félicien Kabuga kupelekwa kwa mahakama ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Rwanda-'International Residual Mechanism for Criminal Tribunals' (IRMCT) mjini Hague.

Félicien Kabuga anadaiwa kuwa mfadhili mkuu wa Wahutu wenye itikadi kali ambao waliuwa watu 800,000 mwaka 1994.

Walikuwa wanawalenga kundi dogo la watu wachache kutoka jamii ya Watutsi pamoja na wapinzani wao kisiasa, hasa kutoka jamii ya Wahutu.

Félicien Kabuga ni mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, ambaye alichukuliwa kuwa mtu tajiri zaidi nchini humo kabla ya kufanyika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Alizaliwa katika eneo la kaskazini mwa Rwanda ambako alijilimbikizia mali kutokana na biasahara ya majani ya chai miaka ya 1970 na kuwekeza katika biashara tofauti nchini humo, mataifa jirani na ng'ambo.

Alikuwa mwandani wa karibu wa chama tawala cha MRND na baba mkwe wa rais Juvénal Habyarimana.

Kabuga anayetuhumiwa kuwa mfadhili mkuu wa mipango ya kutekeleza mauaji ya kimbari , alikuwa mwenye hisa mkuu katika kituo cha radio ya kibinafsi RTLM ambacho kililaumiwa kwa kuwahamasisha watu wa jamii ya Kihutu kuwaua wenzao wa Watutsi.

Kutokana na utajiri wake, baada ya mauaji ya kimbari Kabuga, mwenye umri wa miaka 84, alifanikiwa kujificha katika mataifa mengi hadi alipokamatwa Mei 16,2020.