Chadema kufungua kesi mahakamani baada ya mgombea wake kuadhibiwa na tume ya uchaguzi

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kilimpitisha Tundu Lissu (aliyeinuliwa mkono) kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi ujao wa Oktoba.
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kilimpitisha Tundu Lissu (aliyeinuliwa mkono) kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi ujao wa Oktoba. CHADEMA Tanzania/twitter.com

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kimesema mgombea wake wa urais Tundu Lissu hatafanya kampeni kwa siku saba, ili kutekeleza adhabu aliyopewa na Tume ya Uchaguzi kwa kutoa maneno ya uchochezi.

Matangazo ya kibiashara

Kamati ya Maadili ya Kitaifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imemsimamisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kufanya kampeni kwa muda wa siku saba, kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi.

Taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa na kutiwa saini na Katibu wa Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi ya NEC, Emmanuel Kawishe imesema kamati yake imeafikiana kumsimamisha Tundu Lissu kufanya kampeni za uchaguzi kwa siku saba, kwa kukiuka maadili ya uchaguzi na kutoa lugha ya kichochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni ya 2.1 (a), (b), (d) na (n).

Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema, baada ya kutambua mtego wa Tume, wao kama chama, wameona mgombea wao atii adhabu aliyopewa lakini watafungua kesi Mahakamani.

Kuhusu kuwa na mgombea moja wa urais visiwani Zanzibar na Tanzania Bara, Mbowe amesema chama chao kwa upande wa Zanzibar kitamuunga mkono mgombea wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad.