BURUNDI-UN-HAKI ZA BINADAMU

Burundi: Utata waibuka baada ya Tume ya UN kuhusu Haki za Binadamu kuongezewa muda

Kuendelea kuwepo kwa Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Burundi kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi, kumeendelea kuzua mgawanyiko nchini humo.

Maafisa wa polisi wakipiga doria katika moja ya mitaa ya Bujumbura, tarehe 12 Aprili 2016.
Maafisa wa polisi wakipiga doria katika moja ya mitaa ya Bujumbura, tarehe 12 Aprili 2016. STRINGER / cds / AFP
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Burundi inashtumu Tume hiyo kuongezewa muda, huku wanasiasa wa upinzani wakiunga mkono kuendelea kuwepo nchini Burundi kwa wajumbe hao wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujubu wa balozi wa Burundi katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Rénovat Tabu, azimio la kurefusha muhula wa tume hiyo ya haki za binadamu Burundi ni njama za Umoja wa Ulaya tangu mzozo wa mwaka 2015.

Anasema ni dhahiri kuwa Umoja wa Ulaya uliunga mkono kwa hali na mali makundi ya waandamanaji walioshirikiana na wanasiasa pamoja na askari kwa kujaribu kuipinduwa serekali tarehe 13 Mei mwaka 2015. Amebaini hayo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu, Jumanne wiki hii. Rénovat Tabu amepinga tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuhusu haki za binadamu nchini Burundi.

« Kamwe Burundi haitoshirikiana na tume hiyo. Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya, matatizo ya Burundi si ya haki za binadamu bali ni ajenda ya kisiasa inaodhamiria kupasishwa kwenye Baraza la Haki za Binadamu. Serekali ya Burundi ingependelea kuwajulisha kuwa hali ni tulivu, ila tu inakabiliwa na chokochoko za kidiplomasia tangu mwaka 2014”.

Kwa upande wake Phéneas Nigaba, msemaji wa chama cha Frodebu, cha upinzani nchini Burundi, ameiomba serekali iwaruhusu wajumbe wa tume hio ya haki za binadamu kuingia nchini Burundi.

«Burundi haiwezi kusema kila mara kuwa tume hio sio lazima. Wakati ilipoundwa, chanzo ni machafuko. Je haki za binadamu zinaheshimishwa ? Ikiwa muhula wa tume hiyo umerefushwa, ni kwa sababu ni muhimu. Tunaiomba serekali iwakubaliye wajumbe wa tume hiyo waje Burundi, washuhudiye yanayojiri. Iwapo haki za binadamu hazikiukwe, tume hiyo haitosema zinakiukwa na huku zinaheshimishwa ».

Azimio la kuunda Tume hio ya Umoja wa Mataifa ya Uchunguzi kuhusu haki za binadamu nchini Burundi lilipitishwa tarehe 30 mwezi Septemba 2016, na wajumbe wake bado hawajaruhusiwa kuingia nchini Burundi.