Patrick Amuriat Oboi kupeperusha bendera ya chama cha upinzani cha FDC Uganda
Imechapishwa:
Chama kikuu cha upinzani nchini Uganda FDC, kimemteua kiongozi wa chama hicho Patrick Amuriat Oboi, kupeperusha bendera ya chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Februari mwaka 2021.
Itakuwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho kuwa na mgombea tofauti tangu mwaka 2001, ambapo mwanasiasa mkongwe wa upinzani Kizza Besisgye amekuwa akipambana na rais Yoweri Museveni.
Hivi karibuni Kizza Besigye, ambaye aliwahi kuwania urais mara nne, alitangaza kuwa hatawania tena wadhifa huo wakati wa Uchaguzi Mkuu mapema mwaka 2021.
Besigye ambaye aliwahi kuwa daktari wa maungo wa rais Museveni alimpinga Museveni mara nne katika uchaguzi tangu mwaka 2001 lakini hakuweza kupata nafasi ya kushinda katika chaguzi zote hizo.
Besigye husifiwa sana kutokana na moyo anaoonyesha anapotoa hotuba zake na wengi wamemsifu kwa kusimama na kupinga utawala wa Museveni.
Amuriat anaungana na rais Museveni na Robert Kyagulanyi katika orodha ya wagombea urais, huku akionya kuwa chama tawala NRM kisitarajie kuiba katika Uchaguzi huo.