BURUNDI-HAKI ZA BINADAMU

Burundi: Waliohusika na mauaji ya rais wa zamani Ndadaye wahukumiwa kifungo cha maisha

Rais wa kwanza wa Burundi aliyechaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye, aliuawa Oktoba 21,1993.
Rais wa kwanza wa Burundi aliyechaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye, aliuawa Oktoba 21,1993. ANP/AFP Dabrowski

Mahakama Kuu ya Burundi imetoa uamuzi wake Jumatatu, Oktoba 19 katika kesi ya wale wanaoshtumiwa kuhusika na kushiriki katika mauaji ya rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia, Melchior Ndadaye, mnamo mwaka 1993.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, ambaye kwa sasa ni Mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali, pamoja na viongozi wengine 18 waandamizi, raia na wanajeshi wa jeshi la zamani, wakati huo likitawaliwa na kabila la walio wachache la Watutsi, wamehukumiwa kifungo cha maisha hasa kwa "shambulizi dhidi ya rais wa nchi ".

Viongozi wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kushiriki katika mauaji hayo.

Mtu mmoja tu wa wakati huo amefutiwa mashitaka. Maafisa watano waandamizi wa zamani katika jeshi, ikiwa ni pamoja na wanne ambao wanazuiliwa jela tangu mwaka 2018, wamefikishwa mahakamani wakati hukumu hiyo ilitolewa, na wengine wote wamehukumiwa bila wao kuwapo.

Mawakili wao wamelaani tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo huko Gitega, katikati mwa nchi, utaratibu unaotumiwa katika kesi hiyo wakisema kuwa unakiuka haki za utetezi na vile vile Mkataba wa Amani uliotiwa saini mnamo mwaka 2000 jijini Arusha, nchini Tanzania.