Burundi: AU matatani baada ya kutolewa hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya Pierre Buyoya
Imechapishwa:
Hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya iliyotolewa mapema wiki hii na mahakama nchini Burundi imeuweka matatani Umoja wa Afrika.
Pierre Buyoya ni mwakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika kanda ya Sahel. Umoja aw Afrika haujatoa tangazo lolote kuhusiana na hukumu hiyo, wakati uhusiano unaendelea kudorora kati ya umoja huo na Gitega.
Miaka miwili iliyopita, Umoja wa Afrika ulizungumzia kuhusu suala la waranti wa kimataifa wa kukamatwa uliotolewa na serikali ya Burundi dhidi ya Pierre Buyoya na washtakiwa wenzake, ukiitaka serikali ya Burundi "kujiepusha na hatua yoyote inayoweza kuleta ugumu katika utaftaji wa 'suluhisho la maelewano' nchini.
Waranti huo wa kukamatwa haukuwa na athari kwa rais wa zamani wa Burundi, ambaye sasa ni Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika huko Mali na kanda ya Sahel. Ameeendelea shughuli zake na kusafiri ulimwenguni, kana kwamba hakuna kitu kilichotokea.
Wakati huo huo Pierre Buyoya ameipuuzilia mbali kesi hiyo akisema ilichochewa kisiasa
Pierre Buyoya, ambaye aliongoza Burundi mara mbili na ambaye kila wakati alikabidhi madaraka kwa raia, ni mmoja wa watu mashuhuri wa barani Afrika anayeheshimiwa katika taasisi za kimataifa, licha ya mauaji ya kikabila yaliyoweka dosari katika utawala wake. Hukumu ya kifungo cha maisha dhidi yake inahusiana na mauaji ya Melchior Ndadaye, rais wa kwanza kutoka jamii ya Wahutu aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka 1993.