BURUNDI-BUYOYA-HAKI

Burundi: Rais wa zamani Pierre Buyoya alaani 'kesi ya kisiasa' dhidi yake

Rais wa zamani wa Burundi na mwakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika nchini Mali na kanda ya Sahel Pierre Buyoya (kulia).
Rais wa zamani wa Burundi na mwakilishi mkuu wa Umoja wa Afrika nchini Mali na kanda ya Sahel Pierre Buyoya (kulia). GEORGES GOBET / AFP

Baada ya kuhukumiwa, bila kuwepo mahakamani, kifungo cha maisha, kwa madai ya kuuawa kwa mtangulizi wake mwaka 1993, Melchior Ndadaye, wakati wa mapinduzi ya kijeshi, rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya amelaani uamuzi wa mahakama akibaini kwamba atakata rufaa.

Matangazo ya kibiashara

Katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa Oktoba 23 huko Bamako, nchini mali, Pierre Buyoya ambaye ni mwakilishi Mkuu wa sasa wa Umoja wa Afrika kwa Mali na kanda ya Sahel, amefutilia mbali hukumu hiyo na kutangaza kwamba yuko tayari kukabiliana na uamuzi huo wa kisiasa.

Mbele ya waandishi wa habari, Pierre Buyoya, rais wa zamani wa Burundi alionekana akizungumza bila hasira, na amebaini kuwa kuhukumiwa kwake hivi karibuni nchini mwake kwa kifungo cha maisha kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya mtangulizi wake Melchior Ndadaye ni uamuzi ambao haupi nguvu yoyote kwani ni majaji kuchukuwa uamuzi huo walishinikizwa na viongozi na kuongeza kuwa hiyo ni 'kesi ya kisiasa.'

"Tutakata rufaa kwa mahakama za Burundi na, wakati ukiwadia, tutawasilisha malalamiko yetu mahakama za nje ya nchi, " amesema Pierre Buyoya.

Buyoya amehukumiwa pamoja na watu wengine 18 kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza wa Burundi kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia Melchoir Ndadaye.

Kulingana na mahakama, 19 hao wamepatikana na makosa ya kushambulia kiongozi wa nchi, na kujaribu kusababisha machafuko, mapigano na mauaji ya halaiki ya watu nchini Burundi.

Mashtaka dhidi ya aliyekuwa waziri mkuu Antoine Nduwayo yamefutwa baada ya ushahidi dhidi yake wa kushiriki katika njama hiyo, kukosekana.

Buyoya, ambaye sasa anafanya kazi kama mwakilishi maalum na kiongozi wa ujumbe wa amani wa kimataifa unaongozwa na Afrika - AFISMA, nchini Mali, amekuwa akitafutwa na mamlaka nchini Burundi baada ya kibali cha kimataifa kutaka akamatwe na kupelekwa nchini humo kutolewa mnamo mwaka 2018.

Kibali hicho cha kukamatwa kilitolewa na mwanasheria mkuu wa Burundi Sylvestre Nyandwi, kwa kushukiwa kupanga njama za kumuua rais wa kwanza kutoka jamii ya Hutu, Ndadaye.

Buyoya, ambaye anatoka jamii ya watutsi, ametaja mashtaka dhidi yake kuwa mbinu ya kugawanya nchi na kubadili mawazo ya watu kutokana na matatizo yanayoikumba nchi hiyo.

Ndadaye aliuawa Oktoba 21 1993, siku 102 baada ya kuapishwa kuwa rais wa Burundi.