TANZANIA-ZANZIBAR-UCHAGUZI-SIASA

Upinzani-Zanzibar: Watatu wauawa na polisi Zanzibar katika makabiliano kabla ya uchaguzi

zoezi la upigaji kura ya mapema visiwani Zanzibar linaendelea kwa makundi maalumu tu ya wapiga kura.
zoezi la upigaji kura ya mapema visiwani Zanzibar linaendelea kwa makundi maalumu tu ya wapiga kura. AFP PHOTO / TONY KARUMBA

Watu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika Kisiwa cha Pemba katika visiwa vya Tanzania vya Zanzibar katika makabiliano, chama kikuu cha upinzani Zanzibar kimebaini.

Matangazo ya kibiashara

Hali hiyo inatokea ikiwa imesalia siku moja tu kabla ya Uchaguzi Mkuu Jumatano Oktoba 28.

Hayo yanajiri wakati zoezi la upigaji kura ya mapema visiwani Zanzibar linaendelea kwa makundi maalumu tu ya wapiga kura.

Wakati huo huo kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif amedaiwa kukamatwa kisiwani Zanzibar.

Mgombea urais Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad
Mgombea urais Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad ACT WAZALENDO ZANZIBAR:twitter.com

Maalim Seif alikamatwa na maafisa wa polisi mapema leo katika kituo cha kupigia kura cha Garagara hatua ambayo imeshutumiwa vikali na viongozi wa upinzani.

Chama cha ACT-Wazalendo anachowakilisha Maalim Seif katika uchaguzi huo kimethibitisha kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba mgombea wake alikamatwa na vyombo vya dola wakati akiwa katika kituo cha kupigia kura cha Garagara.

Hata hivyo polisi inadai kwamba haina taarifa zozote kuhusu kukamatwa huko kwa mwanasiasa huyo wa muda mrefu.

Awali upinzani nchini Tanzania uliishtumu Tume ya Uchaguzi nchini humo kwa kupanga kuiba kura kwa kukipendelea chama tawala cha CCM.

Wakati Tume ya Uchaguzi mara nyingi inatuhumiwa kwa kukipendelea chama tawala, upinzani unashutumu kwa kuandaa udanganyifu halisi kabla ya uchaguzi huu, kupitia Daftari la wapiga kura.

Mapema wiki hii Freeman Mbwoe, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, alishutumu kwenye akaunti yake ya Twitter akibaini kwamba kumepangwa udanganyifu mkubwa kupitia Daftari la wapiga kura, akinyooshea lawama Tume ya taifa ya Uchaguzi.

Nae kiongozi wa chama kingine cha upinzani, ACT-Wazalendo Zitto Kabwe pia alithibitisha kwenye ujumbe wa Twitter kwamba karibu wapiga kura 14,000 waliongezwa kwenye Daftari la wapiga kura katika mkoa wa Kigoma, Magharibi mwa nchi, ambapo alichaguliwa kama mbunge.

Rais John Magufuli, mgombea kwa muhulu wa pili kwenye kiti cha urais, anatuhumiwa kwa kuweka utawala "wa kimabavu" nchini Tanzania wakati wa muhula wake wa kwanza. Lakini, licha ya miaka hii mitano ya ukandamizaji, upinzani unaendelea kuwa na wafuasi wengi.