TANZANIA-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi Tanzania: NEC kuanza kupokea matokeo ya uchaguzi usiku

Kituo cha kupigia kura huko Zanzibar, Tanzania, Oktoba 28, 2020.
Kituo cha kupigia kura huko Zanzibar, Tanzania, Oktoba 28, 2020. AFP/Patrick Meinhardt

Mchakato wa kupiga kura nchini Tanzania umefikia tamati, na wasimamizi wa vituo pamoja na mawakala wanatarajia kuanza kuhesabu kura hizo.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi, NEC, kupitia mkurugenzi wake wa uchaguzi, Dr Wilson Mahera, imetangaza kwamba itaanza kupokea matokeo ya uchaguzi kutoka maeneo mbalimbali leo usiku.

Wapiga kura zaidi ya milioni 29 wamepiga kura Jumatano hii, Oktoba 28 kwa uchaguzi wa urais, wabunge na serikali za mitaa.

Wagombea 15 ndio wanawania kiti cha urais katika uchaguzi huo wenye mvutano mkubwa kati ya upinzani na chama tawala. Wawili kati ya hao ni wanawake.

Rais anaye maliza muda wake John Magufuli, aliyechaguliwa mwaka 2015, anawania katika uchaguzi huu kwa muhula wa pili. Uchaguzi huu unafanyika, wakati vikosi vya usalama na ulinzi vimetumwa katika maeneo mbalimbali kuimarisaha usalama zaidi.

Wapinzani wakuu wa Magufuli ni pamoja na Tundu Lissu wa chama cha Cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA na Bernard Membe wa chama cha ACT Wazalendo.

Awali kulikuwa na taarifa za kukamatwa kwa karatasi za kura ambazo tayari zilikuwa zimeshapigwa katika maeneo ya Kigoma ,Tanga na Kawe. Lakini Tume ya uchaguzi, NEC, imekanusha.

Mamlaka nchini Tanzania imeonya dhidi ya kusambaza taarifa za uongo na kuongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wanaokiuka kanuni za mawasiliano.