Mgombea wa upinzani Tanzania Tindu Lissu apinga matokeo ya uchaguzi
Imechapishwa:
Wakati Tume ya uchaguzi Tanzania imeanza kutoa matokeo ya uchaguzi wa wabunge, ambayo yanaonyesha chama tawala cha CCM kimejizolea viti muhimu dhidi ya chama cha CHADEMA, kiongozi wa upinzani Tundu Lissu amepinga matokeo hayo.
Tundu Lissu amesema kuwa uchaguzi huo ulianza kuingia dosari mapema katika kuapisha mawakala ambao ndio waangalizi wa uchaguzi kwa niaba ya chama chao, huku akitoa wito kwa Watanzania kudai haki yao kwa njia ya demokrasia na sio kwa vurugu yoyote.
Wakati huo huo mgombea urais katika visiwa vya Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif na viongozi wengine wa chama hicho wamekamatwa visiwani humo.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amethibitisha kukamatwa kwa Maalim Seif pamoja na viongozi wengine akiwemo Makamu Mwenyekiti Juma Duni Haji na Mjumbe wa Kamati Kuu.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa uchaguzi katika Tume ya taifa ya uchaguzi, Wilson Charles Mahera amesema tume ya Uchaguzi, NEC, imeanza kupokea ripoti za uchaguzi wa rais, na kwamba baada ya kuzihakiki wataanza kuzichapisha muda wowote.
Rais wa sasa John Pombe Magufuli ambaye anawania muhula wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, anapambana na Tundu Lissu wa CHADEMA, ingawa wapo wagombea wengine zaidi ya kumi ambao wanachukuliwa kama wasindikizaji.