TANZANIA-UCHAGUZI-SIASA

Tanzania: Zoezi la kuhesabu kura laendelea, upinzani watishia kuandamana

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatanu wiki hii ambao upinzani umesema ulikumbwa na udanganyifu mkubwa. Hata hivyo upinzani umetishia kufanya maandamano makubwa.

Wapiga kura wakisubiri kupiga kura Zanzibar, Oktoba 28, 2020.
Wapiga kura wakisubiri kupiga kura Zanzibar, Oktoba 28, 2020. AP Photo
Matangazo ya kibiashara

Awali mgombea wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu alitishia maandamano makubwa iwapo kile anachokidai kuwa dosari za uchaguzi kitaendelea.

Upinzani unasema waangalizi wake walifukuzwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura. Kwa upande mwengine chama kingine cha upinzani ACT-Wazalendo kimesema mawakala wake walishuhudia kupokonywa kwa masanduku ya kura na vyombo vya usalama, kujaza kura za ziada kwenye masanduku na wapiga kura kufukuzwa na maafisa waliosema karatasi za kura zilikuwa zimeisha.

Kwa upande wake Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi, NEC, imesema madai hayo hayana msingi wowote.

Wakati huo huo chama cha Mapinduzi CCM kimeshinda uchaguzi wa jimbo la njombe mjini na Mbeya.

Mgombea wa chama hicho Deodatus Mwanyika alimshinda mpinzani wake kutoka chama cha CHADEMA Emmanuel Masonga kwa kura 29,553 dhidi ya kura 5,940.

Mgombea wa Chama cha mapinduzi katika jimbo la Mbeya Tulia Akson ameibuka mshindi katika uchaguzi wa eneo hilo kwa kujipatia kura 75,225 dhidi ya mpinzani wake Joseph Mbilinyi ambaye amepata kura 37, 591.

Hata hivyo zoezi la kuhesabu kura linaendelea. Rais John Magufuli wa chama tawala CCM analenga kushinda muhula wa pili wa miaka mitano akipambana na mpinzani wake mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Tundu Lissu.