TANZANIA-MAGUFULI-SIASA-USALAMA

Uchaguzi nchini Tanzania: Magufuli atangazwa mshindi, upinzani walaani udanganyifu

Rais wa Tanzania John Magufuli anapiga kura katika uchaguzi wa Oktoba 28.
Rais wa Tanzania John Magufuli anapiga kura katika uchaguzi wa Oktoba 28. REUTERS/Stringer

Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania, NEC, imemtangaza John Pombe Magufuli, mgombea urais wa chama cha CCM kwa muhula wa pili wa miaka mitano, mshindi wa uchaguzi wa urais. Lakini upinzani unashutumu mamlaka kwa udanganyifu mkubwa.

Matangazo ya kibiashara

Waangalizi kadhaa pia wamekosoa vikali chaguzi hizi zilizogubikwa na ukandamizaji.

Rais Magufuli ameshinda kwa asilimia 84.39 ya kura.

"Tume ya Uchaguzi inamtangaza John Magufuli wa chama cha CCM, mshindi wa uchaguzi wa urais aliyeibuka kwa kura nyingi, katika uchaguzi huo," Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, NEC, Semistocles Kaijage ametangaza.

Chama cha CCM pia kimejinyakulia viti vingi bungeni kwa kupata viti 264 wakati wa uchaguzi wa wabunge.

Wakati huo huo rais mpya wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, akiwa jukwaani, amesema yuko tayari kufanya kazi kwa kuboresha maridhiano na upinzani. Hussein Ali Mwinyi ameshinda kwa asilimia 76 ya kura. Ni kwa mara ya kwanza rais wa eneo hilo anachaguliwa kwa kura nyingi kama hizo.

Hayo yanajiri wakati viongozi wakuu wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo katika visiwa hivyo wamekamatwa. Chama kilitoa picha zinazoonyesha baadhi ya waliojeruhiwa baada ya kupigwa na vikosi vya usalama. Wengine hawajulikani walipo.

"Sio mfumo wa vyama vingi tena, ni mfumo wa chama kimoja ambao unafananishwa na demokrasia," mtafiti Nic Cheeseman amesema.

Kwa upande wa waangalizi, wanatofautiana. Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Mashariki imesema kuwa uchaguzi nchini tanzania ulifanyika kwa kufuata utaratibu. Kwa upande wake Shirika linalojihusisha na uchaguzi nchini Tanzania, Tanzania Election Watch, limelaani mchakato huo na kusema kuwa mfumo huo unalenga "unarejesha nyuma demokrasia nchini Tanzania. Mchakato ambao ulikuwa chini kabisa ya viwango vinavyozingatia uchaguzi huru wa haki, ulio wazi na wa kuaminika".

Lakini upinzani haujakata tamaa. Umewasilisha kesi kwa Jumuiya ya Madola ukiomba jumuiya hiyo kufutilia mbali uchaguzi huo, kutuma ujumbe wake nchini Tanzania na kusimamisha Tanzania kama mwanachama katika jumuiya hiyo.