KENYA-CORONA-AFYA

Serikali ya Kenya yachukuwa hatua za kukabiliana na mlipuko mpya wa Corona

Maeneo ya burudani kama vilabu vya pombe, vinatarajiwa kufungwa tena nchini Kenya kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona.

Kenya inaendelea kuripoti visa zaidi vya maambukizi ya virusi vya Corona.
Kenya inaendelea kuripoti visa zaidi vya maambukizi ya virusi vya Corona. REUTERS/Njeri Mwangi
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatano, rais Uhuru Kenyatta alikutana na Magavana na Kamati ya dharura inayoshughulikia mbinu za kudhibiti maambukizi hayo ili kupata mwafaka wa pamoja.

''tumeshindwa kuwaongoza raia kufuata na kuheshimu masharti ya kukabiliana na corona yaliowekwa'', alisema rais Kenyatta.

''Sisi kama viongozi hatuna budi kujitolea , lazima tuwaonyeshe watu wetu mwelekeo. Kusimama na kusaidia kukabiliana na mlipuko huu'', rais wa Kenya ameongeza.

Hatua hizi zinatarajiwa kuchukuliwa kutokana na taifa hilo kubwa kiuchumi la Afrika Mashariki kushuhudia maambukizi mapya ya Corona ya watu elfu moja kila siku, katika siku za hivi karibuni.

Hatua nyingine ambazo tayari zimechukuliwa na serikali ya Kenya ni pamoja na kuzuia mikusanyiko ya kisiasa ambayo imekuwa ikiendelea nchini humo.

Katika mikutano hiyo, viongozi wa kisiasi na wafuasi wao, wakiongozwa na rais Uhuru Kenyatta  na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, wamekuwa wakishiriki bila hata kuvalia barakoa wakati mwingine.

Tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza mwezi Machi, Kenya ina maambukizi Zaidi ya Elfu 57 na vifo zaidi ya Elfu moja.